TINDIKALI JANGA LA KITAIFA......


HILI halina mjadala kwamba kwa sasa nchini Tanzania tindikali ni janga la kitaifa kwani ndiyo silaha nyepesi kwa matumizi lakini inayodhuru kuliko nyingine zote, Uwazi limebaini.

Said Mohamed Saad akiwa hospitali.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili, tindikali ina uwezo wa kuunguza mwili wa binadamu kwa asilimua 75 mpaka 95 endapo aliyemwagiwa atalowa vizuri huku wengine wakipona kutokana na maadui kusimama ‘saiti’ mbaya.

Akizungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, mtaalamu mmoja wa kimiminika hicho kinachoogopwa kwa sasa nchini (jina tunalo) alisema tindikali ina caustic.

“Unajua acid (tindikali) ndani yake ina caustic. Kiswahili caustic maana yake ni choma kama moto. Kile kimiminika kinapomkuta mtu mwilini kama hana nguo, ina uwezo wa kumuunguza kwa asilimia sabini na tano hadi tisini na tano, kifo kinaweza kutokea.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Padre wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui, Joseph Mwang'amba, alipofika katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kumpa pole, Mjini Unguja, baada ya kumwagiwa tindikali Mjini Magharibi - Zanzibar.

“Wengi hawajui kinga yake, lakini maji ni kinga kubwa sana ya mtu aliyemwagiwa tindikali asiumie zaidi. Nawaambia wananchi, wakimwona mtu amemwagiwa tindikali tu wawahi kummwagiwa maji ya baridi, nafuu ni kubwa sana kuliko kukimbizwa hospitali, wamkimbize baada ya huduma hiyo,” alisema mtaalam huyo.

Alisema kutokana na hali ilivyo kwa sasa nchini Tanzania, anaoimba serikali itangaze wazi kwamba tindikali ni janga la kitaifa.

“Kwa sasa silaha kubwa ya maangamizi nchini mwetu ni tindikali. Ukipigwa bomu zito utakatika vipande utakufa, lakini tindikali wengi hawafi ila wanaharibika sana ngozi, wanapoteza sura halisi, imefika mahali hata watu wenye fedha zao wanashindwa kutumia fedha hizo kurudisha ngozi hizo kama zamani.

“Tindikali ina tabia ya kuua leya ya pili hadi ya tatu ya ngozi, ndiyo maana mtu akiungua alama haiwezi kuondoka mwilini, inasikitisa sana. Nadhani ni silaha ambayo upatikanaji wake ni rahisi ndiyo maana wengi wanaitumia.

“Unajua wengi siku hizi wanaachana na silaha kama bunduki kwa sababu inatoa mlio wakati wa matumizi, tindikali haitoi mlio. Mara zote, mlio wa kwanza baada ya tindikali kumkuta aliyekusudiwa hutoka kwa mhusika mwenyewe akilalamikia maumivu, maana anajisikia kama anaungua moto,” alisema mtaalam huyo.

Idadi kubwa ya watu nchini Tanzania wamekumbwa na uhalifu huo wa kumwagiwa tindikali hali inayozidi kuibua hofu kwamba, kweli ‘silaha’ hiyo kwa sasa ni janga la kitaifa.

Wahanga wa tindikali wanatoka mikoa mbalimbali ya nchi na hivyo kuondoa wazo kwamba ni tukio la eneo moja tu.

Mfano, waliomwagiwa tindikali na tarehe zao katika mabano ni, mpiga debe wa Chama cha Mapinduzi  wilayani Igunga Mussa  Tesha (Septemba 2011),  Mwenyekiti wa CCM wilaya mpya ya Gairo, Omar Awadhi, (Juni 2013), Shehe Mkuu Wilaya ya Arumeru (Arusha), Said Juma Makamba (Julai 2013), Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Shehe Fadhil Suleiman Soraga (Novemba  2012).

Wengine ni Sheha wa Tumondo (Zanzibar) Mei 2013, Mohamed Omar Said (Mei 2013), wasichana wawili raia wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kristie Trup (18) (Agosti 2013) na Ijumaa iliyopita Padri wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui, Zanzibar, Joseph Onesmo Mwang’amba naye amemwagiwa na anauguza majeraha katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

No comments: