JIJI la Dar es Salaam lina mambo mengi lakini moja ambalo linatisha ni
kugundulika kwa kijiji cha madawa ya kulevya ambacho kipo kando ya
Bahari ya Hindi.
Kijiji hicho ni Kunduchi, nje kidogo ya jiji na uchunguzi umeonesha
kuwa, madawa ya kulevya yenye thamani ya mabilioni ya shilingi yamekuwa
yakikamatwa katika eneo hilo.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na kwa sharti la kutoandikwa majina yao
, walisema matajiri wengi wa ‘unga’ wamekuwa wakitumia eneo hilo
kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni salama kwa shughuli hiyo.
“Hapa Kunduchi ni kando ya bahari, wengi wanatumia majahazi au boti za
uvuvi kuingiza mihadarati hiyo. Wanapoleta madawa yao wanaonekana kama
wanatoa samaki au mizigo mingine ya kawaida lakini kumbe ni madawa ya
kulevya,” alisema kijana mmoja.
Mzee wa siku nyingi wa kijiji hicho alisema anasikitishwa kuona kuwa
kitongoji chao kimekuwa makao makuu ya biashara hiyo haramu ya madawa ya
kulevya na yanauzwa wakati serikali ipo.
“Kuna wakati tulitaka sana kijengwe kituo cha polisi lakini tukaambiwa
kuna matajiri hawataki hilo, hivyo ajenda hiyo ikaisha na wengi
tunaamini matajiri kwa kutumia fedha hawaruhusu kituo cha polisi kuwepo
eneo hilo ndiyo maana hakijengwi,” alisema mzee huyo na kuongeza kuwa
Kituo cha Polisi cha Silver Sands kiko mbali sana.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa watuhumiwa wengi wa madawa hayo haramu wanakamatiwa katika kijiji hicho.
Kwa mfano, Fred William Chande na wenzake wanane waliwahi kukamatwa kwa
madai ya kuwa na madawa hayo aina ya heroin yenye thamani ya shilingi
bilioni 6.4 Februari 21, 2011 na tayari wamefunguliwa kesi namba 1/ 2012
Mahakama Kuu ya Tanzania.
Chanzo kingine cha habari kilidai kuwa hata madawa aina ya Crystal
Methamphetamine kilo 150 yenye thamani ya shilingi bilioni 6.8
walizokamatwa nazo Agness Jerald ‘Masogange’ na Melisa Edward nchini
Afrika Kusini chimbuko lake ni Kunduchi.
Naye Mwanaidi Ramadhan na wenzake wanane wanadaiwa kukamatwa na madawa
aina ya heroin yenye gramu 2,083.3 ambayo thamani yake ni mamilioni ya
shilingi, eneo la Mbezi Beach Kata ya Kunduchi, Dar na tayari polisi
wamewafungulia kesi mahakama kuu ambapo jalada lao ni namba 10/2012.
Walikamatwa Juni 1, 2011.
Naye Ally Murzai Pirbakshy ‘Haji’ na wenzake watatu walikamatwa
wakidaiwa kuwa na madawa aina ya heroin yenye thamani ya mamilioni ya
shilingi na uzito wa gramu 3,053.5 Septemba 7, 2011. Nao wamefikishwa
mahakama kuu na kufunguliwa kesi namba 10/2012.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania,
Kamishna Godfrey Nzowa alipoulizwa juu ya kijiji hicho alisema polisi
wamekuwa wakifanya kazi kubwa kwa kushirikiana na wananchi na matokeo
yake yamekuwa mazuri.
“Yeyote ambaye ana habari juu ya wanaofanya biashara hiyo aje kuniona na
njia ya bahari tunaidhibiti, wasijidanyanye kuitumia kwani kuna wenzao
walifanya hivyo Lindi tukawakamata, ”alisema Nzowa.
No comments:
Post a Comment