Nani akomeshe mateso haya kwa wanawake ; Mke akatwa mkono na mpenziwe
Kuna
mikasa mbalimbali huwatokea watu katika suala zima la mapenzi, kiasi
cha kusababisha baadhi yao kutopenda tena kuingia kwenye jambo hilo
wakiliona kama ni kitu kisichofaa, ingawa ukweli unaweza kuwa sio huo.
“Sitaki tena wanaume, ni watu wabaya, wameniumiza moyo wangu mno,” anasema Hawa Francis, mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam.
Sababu kubwa ni kero ambazo amewahi kuzipata katika suala zima la
uhusiano. Vivyo hivyo wapo wanaume hawataki kuoa, kwa maelezo kuwa kuna
wanawake wamewahi kuwatesa.
Kama wewe ni kati ya watu ambao
umekata tamaa na suala la uhusiano, fahamu kuwa si wewe pekee.Kuna kundi
kubwa la watu wameshatendewa kiasi cha kufanya wasiwe na raha tena.
Mkasa wa mwanamke kukatwa mkono
Ilikuwa Agosti 7, mwaka huu, saa mbili usiku. Ilikuwa ni siku
iliyobadili historia ya maisha yake. Baada ya kuwa katika mapenzi na
mwanaume huyo kwa zaidi ya miaka 17, wakipendana na kuitana majina yote
mazuri unayoyajua yakiwamo kuambiwa ‘mpenzi wangu nakupenda, nikinywa
maji nakuona kwenye glasi’…leo mapenzi yamegeuka shubiri.
Mwanamke huyo, Mchali Kihiyo (35), mama wa watoto sita, aliyepoteza
viungo vyake kutokana na ukatili wa kijinsia uliofanywa na mwanaume
ambaye wamekuwa na uhusiano nae (jina limehifadhiwa).
“Uhusiano
wetu ulikuwa mzuri, hata hivyo kwa sasa naona mambo yamekuwa magumu
kwangu, leo hii mimi sina mkono wa kushoto na nimeondolewa sehemu ya
viungo vyangu vya upande mmoja,”anasema Mchali,akibubujikwa machozi
kutokana na ulemavu alioupata.
Chanzo cha ulemavu
Anasema maisha yao ya uhusiano yalikuwa ya furaha kwa kipindi chote
lakini yamegeuka shubiri baada ya mwanamume wake huyo kuonyesha dalili
ya kutompenda kama awali, hali ambayo anaitafsiri kama labda alikuwa na
mwanamke mwingine.
Mchali, anasema mikasa na mateso ilianza
miaka mitatu iliyopita baada ya kuhisi kwamba mwanamume wake huyo amezaa
na mwanamke mwingine. Ubaya zaidi ulimtokea baada ya mtoto wa huyo
mwanamke mwingine, kutumbukia kwenye kisima cha maji na kisha kupoteza
maisha.
“Kifo cha mtoto huyo, ndicho kilichozaa tatizo hili la
ukatili dhidi yangu na kunisababishia ulemavu, kwa kuwa huyo mwanaume
wangu na huyo mwanamke aliyezaa nae, walidai kwamba mimi ndiyo
nilimtupia majini marehemu mtoto wao ili afe,”anasema mama huyo.
Mchali, anasema mara baada ya msiba wa mtoto kumalizika, mwanamume wake
huyo alihamia kwa mke mdogo lakini akawa anarejea nyumbani na kumtukana
huku akitishia kufanya lolote analofikiri linafaa.
Anasema
baada ya mateso na vitisho kuzidi aliamua kuondoka kwa mumewe huyo toka
mwezi Aprili mwaka huu na kuamua kurudi kwa wazazi wake huku akiwaacha
watoto wake kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi.
Anasema
alilazimika kuwaacha watoto kutokana na agizo la mumewe, aliyekataa
asiwachukue, hivyo akaanza maisha mengine ya upweke bila watoto huku
akiendesha maisha yake kwa biashara ya kuuza samaki.
Anasema
mwanzoni mwa mwezi huu, aliugua malaria na kukaa nyumbani bila kwenda
kwenye biashara zake. Agosti saba mwaka huu, alipata nafuu na kuamua
kwenda kumsalimia kaka yake, anayeishi mbali kidogo na nyumbani kwao na
ndipo yakamkuta yaliyomkuta.
Anaeleza kuwa alikaa kwa kaka yake
hadi muda wa futari wakafuturu na kushangaa simu yake ikiita, kuangalia
ni namba ya mpenzi wake huyo. Alipoipokea, aliulizwa aliko, yeye
alimweleza yuko kwa kaka yake na kumtaka amfuate mnadani akale nyama
kitendo ambacho anasema alipingana nacho.
Anasema baadaye
aliamua kurudi nyumbani na kusindikizwa na wifi yake hadi karibu na
nyumba yao ikiwa ni saa mbili usiku.Walipoagana, ghafla akashangaa
kusikia sauti ya mumewe ikimuita, alipogeuka alimwona, kisha akamuuliza
alikotoka na kumwambia alikuwa kwa kaka yake.
Kipigo na ulemavu
Anasema mara baada ya kumjibu mwanamume huyo alianza kumpiga na
hatimaye alianguka chini na mumewe akatoa panga na kuanza kumkatakata
sehemu mbalimbali za mwili wake.
Hakika hujafa hujaumbika.
Mchali amecharangwa kwa mapanga kuanzia chini ya goti mguu wa kushoto
hadi kwenye makalio, amekatwa sehemu zaidi ya saba mwilini.
Ni kama alitaka kumkata shingo
Anasema kwa namna anavyoona ni kama alidhamiria kumuua akisema kuwa
mara nyingi akiwa na huo upanga alikuwa analenga kumtenganisha shingo.
Alichofanya mama huyo ni kuweka mikono shingoni kuzuia panga, kitendo
kilichosababisha mkono wake wa kushoto kukatwa kabisa.
Mwandishi wa makala haya baadaye alimwomba mwanamke huyo angalau akae
chini, kwani muda mwingi wa mahojiano alikuwa amelala, ndipo alipojibiwa
kwamba hawezi kukaa kwa vile kuna nyama kubwa kwenye makalio ambayo
imeshindikana kushonwa.
Mama huyo anasema wakati mumewe
akimcharanga mapanga, mama yake mzazi aliendelea kupiga ngolo (yowe)
kuomba msaada, kaka yake alikwenda lakini akashindwa kutoa msaada kwa
kuwa shemeji yake huyo alikuwa akimkimbiza na panga.
Anasema
kelele za mama yake zilisaidia kuokoa maisha yake, kwa kuwa majirani
walijitokeza, hivyo mwanamume huyo akaanza kuwakimbiza akitaka kuwadhuru
kitendo ambacho mama huyo aliona ndiyo nafasi pekee kukimbilia ndani.
Matibabu
Mchali, anasema baadaye ndugu zake, walitafuta usafiri na kufanikiwa
kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako alilazwa kwa
siku nne na kurejea nyumbani kutokana na ushauri wa daktari
anayemhudumia.
Kwa mujibu wa mama huyo, daktari anayemtibu
alimtaka Mchali akubali kutibiwa majeraha akiwa nyumbani ili kuepuka
maambukizi ya magonjwa nyemelezi pamoja na kuepuka gharama za matibabu.
“Sina uwezo wa kukabiliana na gharama za matibabu kwa kuwa siwezi
kutembea, nalazimika kukodi gari na kwa wiki naoshwa mara tatu.
Nisaidieni ndugu zangu, ndoa yangu imenifikisha hapa,” anasema.
Mchali na hali ya ukatili mkoani Manyara
Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa anasema mtuhumiwa bado
hajakamatwa kwa vile hajulikani aliko, huku akiahidi kuendelea
kulifanyia kazi suala hilo.
Akielezea zaidi ukatili mkoani
Manyara, anasema upo, japo ni mdogo ikilinganishwa na mikoa mingine.
Anaamini kuwa bado changamoto ni kubwa kwa wanawake ambao wengi wao
wamekuwa wakinyanyasika.
Sababu kubwa za kunyanyasika kwa
wanawake ni mfumodume. Akasisitiza kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo
linaendelea kuelimisha jamii madhara ya ukatili na kusema jitihada hizo
zinapaswa kuigwa na wananchi na asasi nyingine kuhakikisha ukatili wa
kijinsia unatokomezwa.
Msimamo wa wanaharakati
Mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya Kwieco, inayojihusisha na utoaji wa
msaada wa kisheria na haki za binadamu mkoani Kilimanjaro,Wakili
Elizabeth Minde, anasema hali ni mbaya hasa kwa wanandoa wa kike, kwani
wengi ndani ya ndoa hawana nguvu.
Taifa lilipofikia
Hali ya ukatili dhidi ya wanawake nchini bado ni kubwa kutokana na
takwimu zinazoonyesha asilimia 39 ya wanawake wenye umri kati ya mika 15
hadi 49 wanafanyiwa vitendo vya ukatili.
Waziri anena
Naibu waziri wa maendeleo ya jamii jinsia na watoto, Ummy Mwalimu
alikiri ukatili dhidi ya wanawake kuongezeka na kusema vitendo kama
kupigwa na kubakwa ni matukio yanayoongoza zaidi na yanafanywa na
wanaume, huku akisisitiza kuendelea kuangalia namna ya kufanya ili
wanawake nchini waendelee kufurahia maisha.
Safari ya ndoa
Kwa mujibu wa Mwanasaikolojia, Modesta Kimonga anayefanya shughuli zake
za ushauri Mkoani Mbeya, ndoa inaweza kufananishwa na safari ndefu
yenye matukio yasiyotazamiwa, mengine yenye kupendeza na mengine yenye
kuumiza.
Anasema mafanikio katika ndoa hayapimwi kwa panda
shuka za safari bali yanapimwa kwa jinsi wenza wanavyoshughulikia hali
hizo Ndio kusema ni suala la msingi kwa walio kwenye ndoa kujifunza
namna ya kupambana na changamoto zinapotokea, siyo kutesana au
kukimbiana.
Ushauri zaidi
Mshauri maarufu wa ndoa
nchini Uingereza, Hussain Zahid anasema katika makala ya kitabu chake
cha ‘My marriage’ yaani ndoa yangu kuwa msingi wa kuwa na ndoa nzuri ni
kupata muda wa kuzungumza baina ya wanandoa wenyewe ili kuondoa tofauti
zao.
“Kila mtu ajione analo deni la kumpenda na kumfanyia mema
mwenza wake. Kila mtu ajifunze kauli nzuri na matendo mazuri kwa mwenzi
wake…kwamba kabla ya kufanya lolote, tafakari, ungefurahi kufanyiwa hilo
unalotaka kulifanya,” anaonya.
Staili mpya ya maisha kwa baadhi ya wanawake
Tafiti zinaonyesha kwamba kutokana na uwepo kwa mikwaruzo mingi katika
mapenzi, kuna wanawake hawataki tena kuolewa. Kama lengo ni kupata
mtoto au watoto, huwa tayari kuzaa na yeyote hata kama ni mume wa mtu,
kisha jukumu la kulea kwa asilimia kubwa hufanya wao au kwa kushirikiana
na hao waliozaa nao.
Hata hivyo wataalamu mbalimbali wa
masuala ya ndoa, wanashauri watu kuacha tabia hiyo ya kuzaa tu, badala
yake wapende kuzaa wakiwa kwenye ndoa kwa sababu mtoto ambaye hana mzazi
mmoja, huathiriwa sana na matatizo ya kisaikolojia.
Mfano wa utafiti
Kulingana na utafiti uliotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Marekani, uko uwezekano mkubwa wa watoto wenye kulelewa na mzazi
mmoja kuwa na tabia mbaya zaidi ya watoto wenye wazazi wote.
“Kama ni suala la kuiga tabia na matendo mabaya, watoto ambao wana mzazi
mmoja wanaharibika mara tano zaidi ya watoto ambao wana wazazi wote
wawili,” inasema sehemu ya utafiti huo.
Utafiti unaongeza kuwa
hata wanapofika kwenye umri wa ujana, vijana ambao wana mzazi mmoja,
wanaharibika zaidi ya wale ambao wana wazazi wote; Wana uwezekano wa
kuharibika mara tatu zaidi ya vijana ambao wanaishi na wazazi wote
wawili.
Si wote huharibika
Hata hivyo utafiti
unasisitiza kuwa si watoto wote wenye mzazi mmoja huwa na tabia mbaya,
bali kinachosemwa ni kwamba kwa asilimia kubwa watoto wa aina hiyo
huharibika zaidi ya wale ambao wanalelewa na wazazi wote wawili.
Wanaoathirika zaidi ni wale ambao wazazi wao wametalakiana, hasa kwa
sababu mara nyingi hata nguvu za kulea watoto hupungua kutokana na
wazazi au mzazi husika kuwa na msongo wa mawazo.
Matendo mabaya
kama vile ya mzazi mmoja kuteswa na mwingine au mtoto kuona mama au
baba yake akimshtaki mwenzi wake, huchangia kwa kiasi kikubwa kuendelea
kumuathiri mtoto kitabia.Tabia kama za kupigana au mateso mengine kabla
ya wanandoa kuachana, huchangia kuharibu maisha ya mtoto kwa kuona labda
kupigana ndio njia nzuri ya kupambana na mtu anayekukwaza au mwingine
kutishwa na uhusiano kwamba unaweza kusababisha mateso.
Sababu ya migogoro na tiba yake
Mtafiti maarufu wa masuala ya ndoa kutoka Urusi, Korotayev, A, katika
chapisho lake alilolipa jina “Division of Labor by Gender’ yaani
mgawanyiko wa majukumu katika jinsia, anasema msingi wa kuwa na uhusiano
mbaya katika ndoa nyingi ni kutokuwa na fursa ya kukaa pamoja na
kukubali kuondoa kasoro.
“Hakuna mtu ambaye yuko safi kwa
asilimia 100. Umekaa tumboni mwa mama yako na kuna wakati mnagombana,
iwe mtu ambaye mmekutana tu mitaani?”anahoji Korotayev, huku
akiwasisitiza watu walio kwenye ndoa kubuni mbinu za kupendana na
kufanya mikakati mingine ya maisha badala ya kuendekeza ugomvi,
kufikiria kuachana au kutafuta wapenzi wengine