MAMA WA MTOTO ALIYEFUFUKA HUKO GEITA ACHARANGWA MAPANGA NA WATU WASIOJULIKANA.


Mama mzazi wa Shaban Maulidi, Aziza Ramadhan.

WATU zaidi ya 10 wasiojulikana wakiwa na mapanga na nondo waliivamia familia ya mtoto aliyedaiwa kufufuka,

Shaban Maulidi kisha kuwajeruhi kwa silaha hizo watu saba, akiwemo mama mzazi wa mtoto huyo, Aziza Ramadhan, Uwazi lina kisa kamili.

Tukio hilo lilitokea usiku wa saa 9 Jumamosi iliyopita katika Kitongoji cha 14 Kambarage, Kata ya Kalangalala mjini Geita ambapo mama huyo na familia yake walikuwa wamelala ndani.

Inadaiwa watu hao kabla ya kufanya ukatili huo walizizingira nyumba za jirani pia na kuingia moja baada ya nyingine kwa kugonga milango kwa nguvu na kuwashambulia kwa mapanga na nondo wakazi wake huku wakiwalazimisha watoe pesa.

Maneno Sungura ambaye naye alijeruhiwa.


Habazi za ndani zinadai kuwa, watu hao walikuwa wakimtafuta Shaban ili wamuue ikiaminika kuwa, hatakiwi kuishi kwa sababu kifo chake kilikuwa cha kishirikina iweje afufuke, baada ya kumkosa ndipo walipoamua kumjeruhi mama yake kisha kuvamia nyumba za majirani wa familia hiyo wakijua mtoto huyo alifichwa humo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mama, baada ya mwanaye kuruhusiwa kutoka Hospitali ya Wilaya Geita alikolazwa aliondoka na baba yake na kwenda kufichwa sehemu ili kuepusha msongamano wa watu ambao wangefurika nyumbani hapo kumtazama.

Mtoto aliyedaiwa kufufuka, Shaban Maulidi.


Akisimulia jinsi watu hao walivyompora fedha, mwanamke huyo alisema:

“Wakiwa wameshanijeruhi sehemu mbalimbali kwa mapanga na nondo, wakataka hela. Nilikuwa na shilingi elfu kumi nimeifungia kwenye nguo, nikafungua nikawapa, chini ya kitanda nilikuwa na shilingi laki mbili nilizochangiwa na ndugu na jamaa waliokuwa wanakuja kumwona mwanangu hospitali, nazo wakachukua,” alisema Aziza.

Alipoulizwa kama tukio hilo linahusiana na kufufuka kwa mwanaye kama ilivyoenezwa na baadhi ya watu kwamba mtoto huyo hatakiwi kuishi, mama huyo alijibu:

Aziza Ramadhan akiwa na jeraha kichwani.


“Yawezekana maana waliniambia wametumwa kutuua mimi na mtoto wangu lakini wakasema endapo nina pesa niwapatie wasiniue. Kwa hiyo sijui kama lengo lao lilikuwa ni mtoto au la!”

Wengine waliojeruhiwa katika tukio hilo ni Maneno Sungura (36), Peter Kulwa (23) na  Doto Lucas ambaye umri wake haukujulikana mara moja.

Majirani Zachary Petro, Bahati Musa na Samuel Runguya licha ya kujeruhiwa, pia waliporwa zaidi ya Sh. 388,000 na simu moja ya mkononi yenye thamani ya Sh. 45,000. Majeruhi wote walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kupatiwa matibabu na baadaye kuruhusiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Leonard Paulo alipotafutwa kwa njia ya simu na kuulizwa kuhusu tukio hilo hakukiri wala kukanusha kutokea na badala yake alisema: ”Niko sehemu mbaya sana,” akakata simu.

No comments: