WAPINZANI WAUNGANA NA KUKUBALIANA KUFANYA MIKUTANO NCHI NZIMA ILI KUPINGA MCHAKATO WA KATIBA....

 
VYAMA vya upinzani nchini, vimeamua kuungana ili kunusuru mchakato wa Katiba mpya. Msimamo huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam, wakati wenyeviti wa vyama hivyo ngazi ya taifa, walipofanya mkutano na waandishi wa habari.

Vyama vilivyofikia uamuzi huo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilichowakilishwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, Chama cha Wananchi (CUF), kilichowakilishwa na Profesa Ibrahim Lipumba na Chama cha NCCR- Mageuzi, kilichowakilishwa na James Mbatia.

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, aliyesoma tamko lao ni Profesa Lipumba, ambaye alisema ushirikiano wao umelenga kuhakikisha Katiba mpya inapatikana kwa maslahi ya Watanzania.

Alisema kwamba, ushirikiano huo umetokana na Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya kupitishwa bungeni Septemba 6, mwaka huu, kwa nguvu na wabunge wa CCM.

Alisema kuwa, muswada huo ulipitishwa ukiwa na kasoro mbalimbali, zikiwamo za CCM kuingiza vipengele bila kufuata utaratibu kwa maslahi yao na pia wananchi wa Zanzibar hawakushirikishwa ipasavyo.

“Muswada uliopelekwa bungeni, uliongezwa vifungu vingi ambavyo havikuwamo katika rasimu iliyopelekwa katika Serikali ya Zanzibar, kitendo hicho kinadhihirisha udanganyifu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika suala la Katiba ya nchi inayotokana na wananchi.

“Sasa, yaliyojiri bungeni kwa siku tatu kuanzia Septemba 4 hadi 6, mwaka huu na yale yanayoendelea kusemwa na Serikali pamoja na CCM, ni mkakati wa kupitisha Katiba ambayo haikutokana na wananchi. Kwa maana hiyo, wenye nia njema na nchi, waunge mkono tamko hili,” alisema Profesa Lipumba.

Kutokana na kutoridhishwa na mchakato huo, wanasiasa hao walimtahadharisha Rais Jakaya Kikwete, asisaini muswada huo kwa kuwa marekebisho yaliyofanyika na taratibu zilizotumika kuupitisha, zilikwenda kinyume cha majadiliano na vyama na wadau yaliyofanyika mwaka 2011 na 2012.

Pia walimtaka Rais Kikwete kuurejesha muswada huo bungeni, ili ukafanyiwe marekebisho yatakayojenga tabia ya kuaminiana ili kuleta muafaka wa kitaifa wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba.

“Tunaanza kuunganisha umma ili kufanya uamuzi mzito wa kunusuru mchakato wa Katiba mpya, ambao unaendelea kutekwa na kuhodhiwa na CCM na tunafanya hivyo kwa kuwa madaraka na mamlaka yote yapo kwa wananchi ambao Serikali inawajibika kwao,” alisema Profesa Lipumba.

Ili kuonyesha kuwa wapinzani hao hawaridhishwi na mchakato wa Katiba mpya, alisema Septemba 21, mwaka huu, utafanyika mkutano wa hadhara wa pamoja eneo la Viwanja vya Jangwani, Dare es Salaam.

Alisema mkutano huo utakuwa ni hatua ya mwanzo ya ratiba za vyama hivyo kuzunguka nchi nzima kuelezea masuala mbalimbali yanayohusu mchakato wa Katiba mpya.

Akizungumza baada ya tamko hilo, Mbatia alisema kama Rais Kikwete ataridhia mchakato huo haramu, uamuzi wake utakuwa ndiyo chanzo cha machafuko nchini.

Alimtahadhirisha Rais Kikwete asiusaini muswada huo kwa sababu anaweza kuandika historia mbaya ya jambo alilolianzisha kwa nia nzuri.

“Mkono wa Rais Kikwete ambao utashikilia kalamu, ndio utakaokuwa na hatma ya taifa hili, anaweza kujenga historia mbaya ya jambo ambalo amelianzisha mwenyewe, ninamuomba aweke maslahi ya taifa mbele kuliko chama chake.

“Mkono wake ukithubutu kusaini muswada huo, ajue ndio mwanzo wa machafuko, tunajua wapo wanaosema anakiharibia chama chake, lakini ajue tunampa ushauri wa bure ili atambue hagombei tena, hivyo hakuna sababu ya kuogopa mtu.

“Tunataka Katiba ya miaka 50 hadi 100 na ifahamike kwamba, Watanzania hawajawahi kuandika Katiba yao, hatutaki CCM kuhodhi na kuifanya ni mali yao.

“Itakumbukwa kwamba, Muungano wa Tanzania na Zanzibar ni tendo la siasa la maridhiano, hivyo hivyo tendo la Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kati ya CCM na CUF lilifanyika kisiasa na ni la maridhiano.

“Tunaomba CCM waweke itikadi zao pembeni na wote tuseme Tanzania kwanza, siasa baadaye, maslahi ya taifa kwanza, chama baadaye, kwa kauli hiyo, tutapata Katiba mpya.

“Sisi tunashukuru Tume ya Jaji Warioba, kwani imefanya kazi nzuri na kuchukua mawazo ya kila kundi na vyama, yakiwamo ya Serikali tatu, sasa bila vyama vya siasa kuyasimamia haitapatikana Katiba ya Watanzania,” alisema Mbatia.

Mbowe anena

Naye Mbowe alisema haoni sababu uchaguzi wa mwaka 2015, ufanyike chini ya Katiba ya zamani na kuongeza kwamba katiba mpya itapatikana kwa njia yoyote ile.

Mbowe, ambaye alitumia muda mrefu kuwaonya waandishi wa habari, alilifananisha taifa na puto lililojaa upepo ambalo alisema halitakiwi kutobolewa na Rais Kikwete.

Alisema upepo huo ukitobolewa utasababisha machafuko ndani ya nchi na kumtaka Rais Kikwete kutafakari kwa kina kwa kurudisha muswada huo bungeni ili ukajadiliwe upya.

“Chadema hatutaki katiba ya zamani itumike wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015, tutaitafuta Katiba mpya kwa njia mbalimbali hadi ipatikane.

“Tunataka kusonga mbele sio kurudi nyuma, hatutapona kama Katiba mpya hii itapitishwa na chama kimoja, naomba tuungane ili kuwa na sauti moja,” alisema.

Aliwataka waandishi wa habari wawe makini katika suala hili, kwa kuwa wao ni wadau muhimu katika kupata Katiba mpya bora.

Pamoja na hayo, alimzungumzia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira, kwamba amelewa madaraka na kwamba ndiyo maana anatoa kauli za kejeli kwa wapinzani.

Kwa mujibu wa Mbowe, Ikulu siyo mali ya Rais wala wasaidizi wake, bali ni ya Watanzania wote.

Alisema kamwe hawatarajii kwenda Ikulu juu ya suala hilo, bali watakwenda kwa wananchi ambao ndio wenye nguvu na maamuzi ya taifa hili.

No comments: