SAMAKI HATARI WAINGIZWA NCHINI KINYEMELA.


Afya za Watanzania ziko shakani kutokana na kuwapo kwa biashara ya kuingiza samaki kutoka nje ya nchi, wanaodaiwa kuharibika na kuuzwa katika la Soko la Feri jijini Dar es Salaam.

Samaki hao kutoka Yemen, Dubai, China na Japan, wanaoingizwa nchini wakiwa wameganda kwenye barafu, wengi huharibika muda mfupi baada ya barafu kuyeyuka au baada ya kununuliwa.

Uchunguzi umegundua kuwa samaki hao huletwa nchini kutafutiwa soko baada ya kukaa kwenye majokofu kwa muda mrefu huko wanakotoka, kiasi cha kuelekea kuharibika.

Ili wasiharibike, samaki hao aina ya Marckerel hukaangwa hadi wakauke. Uchunguzi zaidi umebaini kuwa wanunuzi wake wakuu ni wafanyabiashara wa chakula wakiwamo wamiliki wa migahawa na Mama Lishe wanaofanya shughuli zao katika miji ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma.

Samaki hao wanauzwa kwa bei ya chini ambayo ni Sh38,000 kwa boksi lenye uzito wa kilo 15, ikilinganishwa na wanaovuliwa hapa nchini ambao bei yake ni Sh60,000, kwa uzito huohuo.

Inaelezwa kuwa samaki hao baadhi yake ni wale ambao wamekwisha muda wake wa kutumika katika nchi hizo, hivyo kuingizwa nchini kutafutiwa soko.

Dk Raymond Mwenekano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anayataja madhara ya ulaji wa samaki wa aina hiyo kuwa ni kupata magonjwa kama vile kansa ya utumbo, mwili kuwasha, kubabuka na vidonda mwilini.

“Madhara yake ni makubwa, ndiyo maana siku zote tunasisitiza kula vyakula visivyokaa sana kwani vingine vimehifadhiwa kwa dawa na wanaofanya hivi ni wafanyabiashara kwa faida yao,” alisema Dk Mwenekano.

No comments: