TUNAENDELEA na mahojiano na staa mkubwa wa Bongo Fleva,
Rehema Chalamila ‘Ray C’ ambaye amepona kutoka kwenye uraibu wa matumizi
ya madawa ya kulevya. Wiki iliyopita alifunguka mambo mengi ambapo
tuliishia pale alipokuwa akizungumzia wimbo wake wa mwisho kabla ya
matatizo. SONGA NAYO…
|
Lord Eyez
|
|
WIMBO WAKO WA MWISHO KABLA YA MATATIZO NI UPI?
“Ni Moto Moto
niliofanya na akina Red Sun na Nonini wa Kenya. Sikuupeleka redioni
nchini Tanzania lakini ukiingia mtandaoni kwenye You Tube utaona
umesikilizwa na kutazamwa na mashabiki zaidi ya 348,142 hadi sasa.
BAADA YA KUTANGAZA KUATHIRIKA NA KUACHA MADAWA YA KULEVYA, NINI KINAKUTESA?
“Hakuna,
najikubali najisikia amani. Nimetua mzigo mkubwa. Watu wananipongeza
kwa ujasiri wangu. Hawanitengi, wananipa sapoti sana. Unajua watu wengi
hawapendi kujitangaza wakiogopa kunyanyapaliwa. Mimi nilijikubali
nikasema bora kusema ukweli ili kuokoa kizazi hiki kinachoangamia kwa
madawa ya kulevya. Na kweli suala la madawa ya kulevya limekuwa ishu
kubwa nchini. Nafurahi kuwa sehemu ya ukombozi wa jamii ya dunia hii.
Siogopi. Kwangu ni tofauti. Mashabiki wangu wananipenda, wananipongeza
mitandaoni. Nimepona na maisha lazima yaendelee.
ULIINGIAJE KWENYE MADAWA YA KULEVYA?
“Kuna mtu alikuwa akiniwekea
bila mimi kujua, sitaki kukumbuka hiyo kitu kitu. Mwanzoni ilikuwa raha
lakini baadaye ikawa karaha na balaa kubwa. Nilikuwa mtu mwenye malengo.
NI NANI ALIKUINGIZA KWENYE MATUMIZI YA MADAWA YA KULEVYA?
“Nilishasema
ni aliyekuwa boyfriend wangu, (anamtaja). Ni Lord Eyez. Nilimpenda sana
lakini najuta kumjua. Arusha wananipenda, wananiita shemeji. Naahidi
kwenda Arusha kuwapa burudani. Nami nawapenda. Niliachana naye mwaka
2010 baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya. Nilimwambia nampenda lakini
ilibidi tuachane. Hakukuwa na namna nyingine. Nilikuwa sijui kama lile
jambo linaweza kuharibu maisha yangu. Mwanzoni alikuwa akiniwekea bila
mimi kujua. Nikaona bora niachane naye ninusuru uhai wangu. Nilikwenda
Nairobi lakini haikusaidia.
ULIKUTANA LINI NA LORD EYEZ?
“(anawaza) Kama sikosei ni mwaka 2008 na tuliachana mwaka 2010.”
UHUSIANO WAKO NA LORD EYEZ UKO KWA SASA?
“Tulikuwa
tukionana tunasalimiana. Sijakutana naye muda mrefu lakini sina ugomvi
naye. Hata tukikutana nitamsalimia vizuri kabisa. Simchukii ila nachukia
madawa ya kulevya. Kama bado anatumia namuombea kwa Mungu aache.
Wenzetu wengi wamekufa, narudia tena, Mungu amnusuru kama bado
anatumia.”
ILIKUWAJE UKASAIDIWA NA JK?
“Baada ya ninyi (Global
kupitia Gazeti la Ijumaa) kuandika kuhusu mimi ndipo Daddy (Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete) akanisaidia,
namshukuru sana kwa kweli. Pia namshukuru Ruge kwa namna
alivyonipigania. Mungu atamlipa.”
UNAWAJUA VIZURI WASANII WANAOTUMIA MADAWA YA KULEVYA, UNAWEZA KUWATAJA AU UNAWAAMBIA NINI?
“Nawajua
(anamtaja msanii mkubwa wa kiume wa Hip Hop Bongo). Anasema hawezi
kuacha lakini mpenzi wake anatumia dozi ya kuacha madawa ya kulevya.
Yeye anamkatisha tamaa. (anawataja wengine) Nawasihi waache watakufa.
Dawa ya kuacha ipo na siyo nje ya nchi, ni Muhimbili (Hospitali ya
Taifa, Dar) tu na huduma inatolewa vizuri sana. Mimi nimepona kwa nini
wao wasipone?”
RAY C KWELI UMEPONA?
“Bado naendelea na dozi. Nimepona lakini si unajua ile kitu inahitaji muda ili kuwa fiti kabisa?”
MARAFIKI ZAKO NI WATU WA AINA GANI?
“Sina tena zile kampani za madawa ya kulevya. Nina marafiki wa tofauti kabisa. Ni watu ambao hawana hizo ishu kabisa.”
UNA HARAKATI ZOZOTE ZA KUHAMASISHA WATU KUACHA MADAWA YA KULEVYA?
“Nafanya
sana. Mtu yeyote nikikutana naye namwambia madhara ya hiyo kitu. Juzi
tu niliweka picha mtandaoni nikiwa na wenzangu walioacha madawa ya
kulevya. Kweli wapo vizuri na nitaendelea kufanya hivyo ndani na nje ya
nchi. Tanzania bila madawa ya kulevya inawezekana.”
BAADA YA MATATIZO RAY C UMEOKOKA?
“No!
Hapana. Mimi ni Mkatoliki lakini nimebatizwa na maji mengi katika
kanisa analosali mama yangu la Sloam lililopo Mbezi Beach, Dar. Siyo
kwamba Katoloki hakuna Mungu ila napenda sana mahubiri ya Sloam.
Yananifariji sana.”
UNAPOWAONA WASANII ULIOKUWA NAO LEVO MOJA WAMEFANIKIWA UNAJISIKIAJE?
“Nina
mafanikio makubwa. Watu wengi wanadhani mafanikio ni kuwa na mali
nyingi. Kwangu ni tofauti. Kuwa na amani tu ni mafanikio makubwa.
Hainipi shida kabisa kuona wao wamefanikiwa badala yake nainjoi sana.”
RAY UNA MCHUMBA?
“Hapana na sihitaji. Kwa sasa najipanga kwanza kwa kazi yangu nzuri ya muziki.”
UNAWAAMBIA NINI WAREMBO JUU YA UCHAGUZI WA WAPENZI WA KUWA NAO?
“Unaweza
kuzaliwa mtakatifu lakini ukafa mwenye dhambi bila kutegemea.
Chondechonde wanawake wenzangu, muwe makini katika kuchagua aina ya
wapenzi mnaotaka kuwa nao maishani la sivyo mtaingia kwenye majanga
makubwa. Mimi nimepita huko ‘so’ chukua hatua.
No comments:
Post a Comment