MTUHUMIWA WA MAUAJI AJIUA KWA KUJIKATA KOROMEO NYUMBANI KWA MWENYEKITI KUKWEPA KUUAWA NA WANANCHI....





Mkazi wa kijiji cha Nyambiti wilayani Chato mkoani geita, Simbi Lugima (35), amejiua ndani ya nyumba ya mwenyekiti wa kitongoji hicho kwa kujikata koromeo kukwepa kuuawa na wananchi wenye hasira, muda mfupi baada kufanya mauaji ya mwanamke mmoja.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana baada ya mtuhumiwa huyo kudaiwa kumuua Yulitha Bilia (57), mkazi wa kijiji cha Nyambiti kwa kutumia panga kabla ya wananchi wenye hasira kumkimbiza kwa lengo la kumuua.
Aliamua kutimua mbio na kujisalimisha nyumbani kwa mwenyekiti wa kitongoji hicho, Zacharia Kanyelema.
Baada ya mtuhumiwa huyo kufika nyumbani kwa Kanyelema, alivamia ndani ya moja ya vyumba vya nyumba ya Kanyelema na kujifungia ndani kabla ya kuamua kujikata koromeo kwa kutumia panga alilokuwa nalo.
Kanyelema alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa huyo alifika nyumbani kwake huku akikimbizwa na wananchi ambapo aliingia ndani ya nyumba yake na kujifungia ili kunusuru maisha yake.
Alisema alilazimika kutuliza hasira za wananchi hao kwa kuwazuia kuvunja nyumba yake kutokana na mtuhumiwa kujifungia humo na kwamba alifanya mawasiliano ya haraka na Jeshi la Polisi wilayani Chato ili kunusuru maisha ya Lugima.
Kanyelema alisema baada ya Jeshi la Polisi kufika eneo la tukio kisha kuingia ndani ya nyumba hiyo, walimkuta Lugima ameshakufa kwa kujikata koromeo.
Baadhi ya mashuhuda waliliambia NIPASHE kuwa chanzo cha kijana huyo kumvamia Bilia na kumuua kwa kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake ni kutokana na mgogoro wa ardhi waliyokuwa wakigombea kwa kipindi kirefu.

No comments: