BUNDUKI ZATENGENEZWA MITAANI...
KIKOSI cha Kuzuia Ujangili cha jijini Dar es Salaam (KDU), kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani hapa, wamegundua mahali kilipo
kiwanda cha kutengeneza bunduki na kuzikarabati kinyume cha sheria.
Kiwanda hicho kiligunduliwa juzi katika Mtaa wa Kingo, Manispaa ya
Morogoro, kutokana na msako uliofanywa na kikosi hicho.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Morogoro,
Faustine Shilogile, alisema kiwanda hicho kiligundulika Septemba 14,
mwaka huu, saa sita mchana.
Pamoja na kugundua kiwanda hicho,
alisema watu sita walikamatwa na watano wanaendelea kutafutwa kutokana
na kujihusisha na utengenezaji wa silaha hizo.
Alisema kiwanda hicho bubu kilikuwa kwenye nyumba ya Ally Mavumila, ambaye ni marehemu.
Alisema
kwamba wakati wa upekuzi katika nyumba hiyo, walikamata vitu mbalimbali
na bunduki 11, zikiwamo aina ya rifle saba, shotgun mbili, magobole
mawili na risasi 22 za rifle.
Alivitaja vitu vingine
vilivyokamatwa kuwa ni maganda 13 ya risasi, mitutu 23, ikiwamo ya
magobole miwili, shotgun miwili na rifle 458 pamoja na vifaa vingine vya
bunduki.
Kwa mujibu wa Kamanda Shilogile, wakati wa upekuzi huo
pia walikamata, mifuko ya kubebea silaha, mkanda wa kubebea bunduki,
vyuma vya kushindilia baruti kwenye magobole, baruti robo kilo pamoja na
mitambo ya kutengenezea bunduki.
Alisema licha ya watu hao
kujishughulisha na utengenezaji wa silaha, pia watuhumiwa hao walikuwa
wakichonga funguo za aina mbalimbali, zikiwamo za magari, pikipiki na za
majumbani.
Hata hivyo, hakuwataja majina, kwa kile alichosema
kuwa, uchunguzi bado unaendelea, japokuwa watafikishwa mahakamani wakati
wowote baada ya upelelezi kukamilika.
Pia, kamanda huyo wa polisi aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano walioutoa na kufanikisha kukamata wahusika wa kiwanda hicho.
Kwa
upande wake, Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Selous, Kisiro Nsabo,
alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya majangili ambao wana
kawaida ya kuua wanyama bila vibali.
“Tuna changamoto kubwa ya
kukabiliana na hawa majangili, kwani tukiwakamata wanasema wametumwa na
matajiri wakubwa, hawa matajiri ndio wanasababisha huu ujangili uendelee
kuwapo, ingawa tunajitahidi kukabiliana nao.
“Kuhusu msako
tulionao, huu ni endelevu na ni maalumu, kwani umeshirikisha Hifadhi za
Mikumi, Milima ya Udzungwa, Selous na Kikosi cha Kuzuia Ujangili kutoka
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment