Lionel Messi alipa kodi aliyokwepa

Lionel Messi

Lionel Messi

Lionel Messi -nyota ya Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina pamoja na babake wamelipa euro milioni tano(sawa na dola milioni 6.6) deni la kodi kabla ya kukabiliana na mashtaka ya kukwepa kodi kwa njia za ujanja, kwa mujibu wa uwamuzi wa jaji mapema leo Alhamisi.

Madai haya ya kukwepa kodi yaliyowasilishwa mahakamani mapema mwezi juni yalikua pigo kubwa kwa hadhi ya mcheza soka huyu ambaye kabla ya hapo alionekana kama mnyenyekevu asiye mizengwe ukimlinganisha na mtani wake mkuu Cristiano Ronaldo mwenye mbwembwe.

Maamuzi ya jaji huko Gava, kwenye pwani ya bahari Mediterenian karibu na mji wa Barcelona, amesema kua babake Messi Jorge Messi alilipa euro milioni 5.02 kwenye mahakama tarehe 14 mwezi Agosti kufidia kodi inayodaiwa haikulipwa pamoja na riba.

Jaji huyo amepinga ombi la mwanasheria wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kutaka alipe kwa dhamana ya hisa ili kuhakikisha kua riba yoyote itakayosababishwa na kesi inalipwa.

Jaji alisema kua haina haja kwa sababu ya uwezo alio nao Bw.Lionel Andres Messi Cuccittini akiongezea kua tayari kodi hiyo imeisha lipwa.

Suala ambalo jaji huyo amesema bado anashauriana na mwanasheria wa upande wa mashtaka ni kuhusu ombi la Messi kutaka kusikilizwa kwa kesi hiyo kuahirishwe kutoka tarehe 17 septemba.

Mashtaka dhidi ya Messi na babake Jorge ni kuhusu kuibia kodi inayotokana na mapato ya biashara zinazotumia sura yake kuanzia mwaka 2006 na 2009.

Inadaiwa kua Messi na babake walijaribu kulihadaa taifa kwa kuhamisha hati miliki za malipo hayo kwenye makampuni yaliyo nje kama huko Belize na Uruguay ili wasilipe kodi nchini Uhispania.

Mawakili wa Messi Juarez Veciana, wamesema kua mteja wao anakubaliana na sheria za Uhispania na yupo tayari kulipa kila fedha anayotakiwa kulipa.

Ufanisi wa Messi uwanjani umemfanya kua mmoja ya sura zinazouzika duniani akiwa namba 10 kwenye orodha ya Forbes miongoni mwa wana michezo mashuhuri wenye mapato makubwa akikadiriwa kupokea dola milioni 21 kila mwaka kutokana na matangazo ya biashara peke yake.

No comments: