MSHAHARA WA RAIS KAA LA MOTO..SEREKALI YASEMA ZITTO ALIKOSEA KUTAJA MSHAHARA WA MTU.

Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kutaja hadharani mishahara ya Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, serikali imekataa kuizungumzia mishahara hiyo.


Msimamo wa Serikali kutotaja mishahara ya viongozi wakuu unatofautiana na utamaduni wa nchi nyingine kama Marekani, Afrika Kusini, Ufaransa na Kenya ambazo mishahara ya wakuu wake huwekwa wazi kwa umma.

Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema akiwa wilayani Igunga Mkoani Tabora, alisema Rais Kikwete anapokea zaidi ya Sh30 milioni kwa mwezi (sawa na Sh360 milioni kwa mwaka) ikiwa ni marupuru na mshahara kwa mwezi bila kodi, huku Pinda akipokea Sh 26 milioni kwa mwezi.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani alisema kiongozi yeyote haruhusiwi kutaja mshahara wa mtu mwingine kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria ya utumishi wa umma.

“Kuutaja mshahara wa mtu mwingine ni kinyume cha sheria na kosa, siyo utaratibu. Kwani wewe upo tayari watu waujue mshahara wako?” alihoji.

Aliongeza kuwa ingawa mishahara ya viongozi hao inatokana na kodi za wananchi, sheria ndiyo inayozuia watu kuyataja malipo hayo hadharani na kwamba hayupo tayari kuutaja mshahara wa rais au kiongozi mwingine labda mtu huyo autaje yeye mwenyewe.

“Siwezi kutaja mshahara wa bosi wangu wala wa kwangu mwenyewe. Wewe unaujua mshahara wa Obama (Rais wa Marekani)?” alihoji tena.

Akizungumzia mishahara ya marais wa nchi nyingine duniani kuwekwa wazi, Kombani alisema kila nchi ina utaratibu wake na kwamba Tanzania haijafikia hatua hiyo.

Alipotafutwa kulizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa. Gazeti hili pia liliwasiliana na Naibu Mtendaji Mkuu mwenye jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo Ofisi ya Rais Ikulu, Peniel Lyimo ambaye alisema yeye si mhusika. “Masuala yote yanayohusu utumishi yapo Wizara ya Utumishi,” alisema Lyimo.

Akianika mshahara wa Waziri Mkuu, Zitto alisema kwamba kiongozi huyo analipwa Sh11.2 milioni kama mbunge, Sh8 milioni kama waziri na Sh7 milioni kwa nafasi yake ya Waziri Mkuu, hivyo, kumfanya kupokea zaidi ya Sh300 milioni kwa mwaka.

Hata hivyo, Kombani alilionya gazeti hili kuandika taarifa za mishahara ya watu kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ally alisema Mwalimu Nyerere aliwahi kutaja mshahara wake hadharani na kuhoji viongozi wanaotaka mishahara yao isitajwe wanaficha nini


“Hata wakificha mishahara yao bado wananchi wataona maisha wanayoishi kuwa si safi,” alisema.



Wanaharakati pia wahoji

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema siyo kosa kwa mtu yeyote kutangaza mshahara wa viongozi wa umma kwa kuwa wanalipwa kutokana na kodi za wananchi.

Aliongeza kuwa kuanzisa sasa atakuwa balozi wa kutangaza mishahara ya viongozi hao, ili kila mwananchi aweze kufahamu kama ambavyo imekuwa ikifanyika katika nchi nyingine duniani.

“Ninachojua mimi ni kuwa dhana ya mshahara inataka kuwepo na siri baina ya mwajiri na mwajiriwa, lakini si kwa viongozi wa umma ambao wanalipwa na kodi za wananchi. Kuanzia sasa hivi nitakuwa balozi wa kutangaza mishahara ya viongozi hao ili kila mtu ajue,” alisema Kibamba.

Katibu Mkuu wa Tanzania Labor Party (TLP), Jeremiah Shelukindo alisema ni vyema kila mtu akaheshimu sheria inayozuia kutaja mshahara wa mtu mwingine kwa kuwa kitendo hicho kinaweza kuwaudhi baadhi ya viongozi wa umma.

“Si vizuri kuingiza siasa kwenye mambo ya mishahara. Siyo mara ya kwanza kusikia watu wakijaribu kutaja mishahara ya watu wengine huko ni kukiuka sheria,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa asasi ya Sikika, Irenei Kiria alisema umefika wakati ambapo inabidi uanze kufanyika mchakato wa kuzibadili sheria zinazolenga kulinda masilahi ya viongozi wa umma.


“Tunataka kujua viongozi wanalipwa shilingi ngapi na kwa nini wanalipwa kiasi hicho,” alisema Kiria.


Nchini Marekani, mshahara wa rais unajulikana tangu mwaka 1789 kiongozi wa nchi hiyo alipokuwa analipwa Dola 25,000 kwa mwaka.

Kuanzia 2001 hadi sasa, Rais wa Marekani analipwa Dola 400,000 (Sh 640 milioni) kwa mwaka, sawa na Sh 53.3 milioni kwa mwezi.

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma analipwa Randi 2 ,917 038 sawa na zaidi ya Sh400 milioni za Kitanzania kwa mwaka, Rais wa Ufaransa, Francois Hollande Sh475 milioni, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron Sh338 milioni, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya Sh277 milioni na Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba Sh226 milioni kwa mwaka.

Wengine na malipo wanayopata kwa mwaka ni Marais wa Urusi, Vladimir Putin, Sh174 milioni, Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia Sh137 milioni, Michael Satta wa Zambia, Sh126 milioni, Rais wa Angola, Jose dos Santos Sh91 milioni, Rais wa Lesotho, Profesa Pakalitha Mosisili Sh88 milioni, Armando Guebuza wa Msumbiji, Sh84 milioni na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping Sh60 milioni.


Wengine ni Rais wa India, Pranab Mukherjee Sh49 milioni, Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe Sh27 milioni, Naibu Rais wa Afrika Kusini, Kgalema Mothlanthe Sh331 milioni, Waziri Mkuu wa Namibia, Nahas Angula Sh160 milioni, huku Baba Mtakatifu wa Kanisa la Romani Catholic, Papa Benedict XVI akifanya kazi bila kulipwa mshahara.

No comments: