WANAFUNZI 300 ELIMU YA JUU KUKOSA MIKOPO.
Zaidi
ya wanafunzi 300 wa elimu ya juu wa vyuo mbalimbali watakosa mikopo
kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kutokana na
kushindwa kujaza fomu za kuomba mikopo katika kipindi kilichowekwa.
Watakaokosa
mikopo hiyo kwa mwaka wa masomo wa 2013/2014 ni kuanzia mwaka wa pili
na kuendelea, ambao hawakujaza fomu za kuonyesha taarifa zao mpya kwa
bodi.
Wanafunzi hao walitakiwa kuwasilisha maombi ya kupewa mikopo kati ya Mei hadi Julai 30, mwaka huu.
Mkugenzi
Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HELSB, Cosmas Mwaisobwa,
aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi
kuhusu utendaji wa kazi wa bodi hiyo.
Mwaisobwa
alisema kwa kuwa wanafunzi hao hawakujaza fomu za kuomba mikopo, mwaka
huu hawatapata fursa hiyo na kwamba kwa mujibu wa utaratibu wao, kila
mwaka lazima mwanafunzi aombe.
Alisema
wanafunzi watakaokosa fursa hiyo ya mikopo wameanza masomo yao katika
vyuo mbalimbali nchini na kwamba HESLB haijui sababu zilizowafanya
wasiombe.
Kuhusu
ufanisi katika utoaji wa mikopo, Mwaisobwa alisema idadi ya wanafunzi
wanaoomba mikopo imeongezeka kutoka 42,729 mwaka 2005/2006 hadi kufikia
wanafunzi 97,348 mwaka 2012/2013.
Aidha,
Mwaisobwa alisema bajeti ya kuwakopesha wanafunzi imeongezeka kutoka
Sh. bilioni 56.1 mwaka 2005/2006 hadi kufikia Sh. bilioni 306 mwaka
20012/2013.
Alisema
mwaka huu serikali imeitengea bodi hiyo Sh. bilioni 325 kwa ajili ya
kuwakopesha wanafunzi wapya, 31,647 na 62,376 wanaondelea na masomo yao
katika vyuo mbalimbali.
Wakati
wanafunzi hao wakikosa fursa ya mikopo, mapema mwezi huu, Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, aliitaka bodi hiyo
kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi na weledi mkubwa kwa mwaka huu wa
masomo ili kuepusha migogoro ya wanafunzi kuhusu mikopo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment