BABU WA LOLIONDO AIBUKA TENA.AINENEA MAZITO TANZANIA.AMWELEZA PINDA MAMBO ALIYOOTESHWA NA MUNGU.
MCHUNGAJI
Ambilikile Mwaisapila wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT) amesema Mungu ameendelea kujifunua kwake na kumuonyesha kuwa
Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na baadaye kioo cha dunia.
Ametoa
kauli hiyo jana asubuhi (Jumanne, Septemba 24, 2013) mbele ya Waziri
Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Samunge,
wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati msafara wa Waziri Mkuu
uliposimama nyumbani kwake ili kumsalimia akiwa njiani kurejea mjini
Arusha.
Mchungaji
Mstaafu Mwaisapila maarufu kama Babu wa Samunge alisema kuna mambo
mengi ambayo yameandikwa kwenye Biblia lakini hayakutokea Israeli na
sasa yatafanyika hapa Samunge. “Mungu ametupenda sana, yanakuja mambo
makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi ni mzee na nitayaona, kwa hiyo
mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema
katika mafunuo aliyopewa na Mungu ameonyeshwa kwamba watu wengi zaidi
watafurika kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa hapo awali. Alitumia fursa
hiyo kuishukuru Serikali kwa misaada iliyotoa wakati wa ‘kugawa
kikombe’ ikiwemo mahema, maji na ulinzi.
Waziri
Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo
ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa za
Ngorongoro, Loliondo na Sale alisema anakubaliana na utabiri wa Mch.
Mwaisapila kwani Tanzania imejaliwa gesi nyingi na mafuta mengi ambavyo
vitabadili sura ya Taifa hili.
“Mungu
ametupa gesi nyingi sana, katika miaka miwili tutakuwa na umeme kila
mahali. Tuna makaa ya mawe ambayo ni nishati kubwa na sasa tuna fursa ya
kupata nishati ya umeme kutoka ardhini (geo-thermal) katika Ziwa
Natron,” alisema.
Alisema Tanzania imekuwa kimbilio la kila mwekezaji na sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo nchini.
Aliwaeleza
wakazi wa Samunge kwamba mapema mwakani mkandarasi wa barabara atakuwa
katika eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ambapo awamu ya
kwanza itaanzia Wasso hadi Mto wa Mbu kupitia Samunge.
Akitoa
ombi maalum kwa niaba ya vijana mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Elias
Kalumbwa alisema wanaomba kuchimbiwa bwawa ili waweze kujiajiri kupitia
kilimo cha mbogamboga na matunda.
Bw.
Kalumbwa ambaye amesomea masuala ya wanyamapori alisema eneo la
kuchimba bwawa lipo katika mto wa msimu unaopita kijijini hapo. “Eneo la
kuchimba bwawa lipo katika mto wetu, vijana tunaweza kujiajiri endapo
tutapata bwawa ili tufanye kilimo cha umwagiliaji maji,” alisema huku
akishangiliwa.
Naye
Bibi Martha Sereri (70) alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanaomba jimbo la
Ngorongoro ligawanywe kwa sababu ni kubwa sana kiasi kwamba inamuwia
vigumu mbunge wao kufika maeneo yote. Aliomba pia wapatiwe walimu wa
sayansi na hisabati kwa ajili ya shule 10 za sekondari zilizopo kwenye
tarafa yao.
Aliomba
wapatiwe mikopo ya matreka ili waweze kuongeza ukubwa wa mashamba yao.
“Tunaomba mikopo ya matrekta na plau, haya mashamba umeyaona njiani
yamelimwa na Wakenya. Ukikodisha trekta kila ekari unatozwa sh.
100,000/-. Je tutafika wapi? Mkitukopesha matrekta mtakuwa mmetusaidia
zaidi,” alisema.
Akijibu
hoja hizo, Waziri Mkuu alisema hoja zao ni za msingi na kwamba suala la
vijana kupatiwa bwawa ni jambo linalowezekana kupitia mipangpo ya
maendeleo ya kilimo ya wilaya (DADPS).
“Andaeni
andiko lenu, inabidi litoke kwa wananchi na siyo Serikalini. Mkituletea
ni jambo linalowezekana kwani liko ndani ya mipango ya wilaya.”
Akijibu
hoja kuhusu ukubwa wa jimbo, Waziri Mkuu aliwaambia wakazi hao kwamba
inawezekana kuongeza jimbo isiwe suluhisho la matatizo yao kwa sababu ya
jiografia ya eneo lao.
“Kuongeza
jimbo inaweza isiwe jibu la kila kitu kwani matatizo mnayopata
yanatokana na jiografia ya eneo lenu, kutoka Ngorongoro, Loliondo hadi
huku Sale. Mimi nadhani tuangalie pia uwezekano wa kuwapa Halmashauri
ili kusogeza huduma kwa wananchi. Tutaangalia njia zote mbili na kuona
ipi italeta majibu ya haraka kwenu,” alisema.
No comments:
Post a Comment