BAADA YA KENYA SASA AL-SHABAAB YAIGEUKIA TANZANIA....WATISHIA KUIVAMIA MUDA WOWOTE KUANZIA SASA..!!
*Yajigamba kufanya mashambulio muda wowote
*Watanzania wapewa mafunzo ya ugaidi nje ya nchi
*Polisi nchini wasema vyombo vya ulinzi viko macho
*Mtanzania akamatwa Kenya akihofiwa gaidi
WAKATI
wananchi wa Afrika Mashariki wakijawa na hofu ya mashambulio
yanayopangwa kufanywa na vikundi vya ugaidi vya Al Qaeda na Al Shabab,
imebainika kuna Watanzania waliopewa mafunzo ya ugaidi wanaojiandaa
kufanya maovu.
Hayo yamebainika siku chache baada ya wanamgambo
wa kundi la Al Shabab kufanya mashambulio katika Jengo la Biashara la
Westgate mjini Nairobi na kuua watu zaidi ya 70 na kuacha mamia wengine
wakiwa wamejeruhiwa.
Mkuu wa Interpol Tawi la Tanzania, Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile aliyasema hayo jana katika
mahojiano maalumu na MTANZANIA.
Alikuwa akizungumzia kauli ya hivi karibuni iliyotolewa na Msemaji
wa Al Shabab, Sheikh Abdulaziz Abu Muscab aliyetoa tahadhari kwamba
kundi lake linapanga mashambulio mengine Tanzania na Uganda.
Babile
alisema taarifa zinaonyesha vijana wa Tanzania waliojiunga na mafunzo
ya ugaidi yanayotolewa na vikundi vya Al Qaeda na Al Shabab, wamefanya
hivyo baada ya kushawishiwa watapata utajiri wa haraka.
Alisema hali hiyo imevifanya vyombo vya ulinzi na usalama nchini kutoipuuza kauli hiyo ya Sheikh Abdulaziz Abu Muscab.
“Tunajua
wapo Watanzania wanapewa dozi za ugaidi, na sisi siyo kisiwa, watu ni
hao hao… tumejipanga kuyakabili haya na kuushirikisha umma katika
ulinzi,” alisema.
Babile alisema kauli ya msemaji wa kundi la Al
Shabab ya kuivamia Tanzania siyo ya kupuuza na kusisitiza kuwa vyombo
vya ulinzi na usalama nchini viko tayari kukabiliana na lolote
litakalotokea.
“Tumeisikia kauli yake kwenye mitandao ya jamii,
imetufanya kuwa alert (macho) vya kutosha, imetuweka sawa na
imetukumbusha kuwa tunaweza kuvamiwa wakati wowote.
“Hatuja-relax
hata kidogo, tumejiweka sawa kwenye human resources zetu, materials
resource na hata frontline officers wetu wako makini mno.
“Mfano
kwenye viwanja vya ndege ambako ni muhimu, kuna mitambo inayoweza
kugundua hati za kusafiria za washukiwa wa uhalifu wanaotafutwa
kimataifa na tutawakamata tu.
“Lakini hata kwenye mipaka yetu
yote hatuko peke yetu, tumepanua wigo wa kupata taarifa za
kiintelijensia na katika kufanya kazi hii tunashirikiana na vyombo vyote
vya ulinzi na usalama,” alisema.
Baada ya kufanya mashambulio
mjini Nairobi Jumamosi iliyopita, Msemaji wa Al Shabab, Sheikh Abdulaziz
Abu Muscab, aliripotiwa kwenye mitandao ya jamii akisema shambulio hilo
lilikuwa ni la kulipiza kisasi baada ya majeshi ya Kenya kuvamia kundi
hilo lenye makazi yake mjini Kismayu, Somalia.
Mitandao ya jamii
pia ilimnukuu Sheikh Abu Muscab akijigamba kuwa wakati wowote
mashambulio ya kikundi hicho yataelekezwa Uganda na Tanzania.
Wakati huohuo, Babile amesema Mtanzania mmoja alikamatwa Kenya akishukiwa kuwa ni mmoja magaidi waliovamia jengo la Westgate.
Bila
kumtaja jina, alisema mtu huyo ni mkazi wa Arusha na alikamatwa muda
mfupi baada ya kuingia Kenya akitoa Tanzania, akitumia usafiri wa mabasi
ya abiria.
“Walipomkamata wakatuletea taarifa sisi, tukatafuta
kwenye database zetu na information za ndani zikatuonyesha hakuwa mtu
hatari, tukamuachia.
“Kilichowatia hofu na kumshuku mtu huyu ni
muda alioingia Kenya na muda wa tukio lilipotokea… lakini tumeangalia
taarifa zote tukagundua hakuwa na shaka,” alisema Babile.
-Mtanzania
No comments:
Post a Comment