TANZANIA YATENGWA RASMI NA EAC.....!
HATIMAYE Tanzania imewekwa kando rasmi na nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC), katika kuunda Shirikisho la Kisiasa
litakaloziongoza nchi hizo.
Tayari marais wa nchi hizo, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni
wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Pierre Nkurunzinza wa Burundi
wamekwishafikia makubaliano ya kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa
Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la nchi wanachama wa EAC, bila
kuishirikisha Tanzania.
Waziri wa Serikali za Mitaa wa Rwanda,
James Musoni, amekaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akieleza
kuwa makubaliano ya kuanzishwa kwa mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya
Katiba ya Shirikisho la Afrika Mashariki, yalifikiwa Septemba 12 mwaka
huu, mjini Kampala na marais wa Rwanda, Kenya na Uganda na hivi karibuni
Rais wa Burundi ambaye alialikwa katika mkutano huo na kushindwa
kuhudhuria, naye sasa amethibitisha ushirika wake katika shirikisho hilo
jipya.
Gazeti la The Sunday Times la Rwanda, limemnukuu Waziri Musoni kuwa marais wa nchi hizo wamekubaliana kukamilisha rasimu hiyo ndani ya muda mfupi.
Musoni
ambaye alikiri kushiriki katika mkutano wa marais hao ulioshirikisha
pia maofisa waandamizi wa nchi hizo isipokuwa Tanzania, alisema uamuzi
uliofikiwa katika mkutano huo ambao ni wa pili kufanyika, ni moja ya
maagizo ya uamuzi uliofikiwa kwenye mkutano wa kwanza uliofanyika pia
mjini Kampala.
“Tumekubaliana juu ya kanuni za kisheria na mpango
mzima utakaotuongoza ili kupata Rasimu ya Katiba itakayoliongoza
shirikisho hilo la kisiasa,” alikaririwa Musoni.
Alieleza kuundwa
kwa kikosi kazi maalumu kitakachojulikana kwa jina la High Level Task
Force (HLTF), ambacho kitajumuisha wataalamu wa nyanja mbalimbali
watakaoandika Rasimu hiyo kwa namna ile ile ya ulivyoandaliwa mpango wa
Itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Musoni
alisema mawaziri wa nchi wanachama waliopangiwa kushughulikia
shirikisho hilo, wanatarajiwa kuelezea mwelekeo wa mafanikio ya mpango
huo katika mkutano mwingine uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi
Oktoba huko Kigali Rwanda.
Kwa mara ya kwanza, marais Kagame,
Museveni na Kenyatta walikutana kufikia makubaliano ya kuharakisha
uundwaji wa shirikisho la kisiasa kwa nchi zao kwa kuondoa vikwazo vya
kiuchumi na kuweka hati ya vitambulisho vya pamoja na ushirikiano wa
kibiashara sambamba na kuzindua mradi wa ujenzi wa gati ya Bandari ya
Mombasa.
Waziri Sitta ashangaa
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta, alipoulizwa kuhusu hatua ya nchi hizo kuanza
kuitenga Tanzania kuelekea kwenye Shirikisho la Kisiasa, alisema Katiba
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ibara ya 7 (e) ya mkataba inaruhusu nchi
wanachama kufanya jambo la haraka kama nchi nyingine zinachelewa
kufanya hivyo.
Sitta alilieleza MTANZANIA Jumatano kuwa, taratibu
za Tanzania haziruhusu kibali cha utambulisho kutumika katika nchi zote
wanachama, kwa sababu lazima raia wa nchi wanachama anapoingia Tanzania
kufuata taratibu za uhamiaji.
Alisema licha ya hatua
zinazochukuliwa na nchi wanachama wa EAC za kuitenga Tanzania katika
baadhi ya mambo, itabakia na msimamo wake na haitakubaliana kuingia
kwenye Shirikisho la Kisiasa huku masuala ya ushuru wa forodha, soko la
pamoja na sarafu moja, hayajatengamaa.
“Huo ndio msimamo wa
Tanzania, hivi vitu vinne vilikuwa bado havijakamilika, matumizi yake
hayajaenda sawasawa na makubaliano ya kila nchi sasa wanaharakisha
Shirikisho la Kisiasa, waache waende kwa sababu Katiba inawaruhusu na
wana ajenda zao za siri.
“Hatuoni suluhisho katika suala hilo, ni
vigumu kuanza kusuluhisha matatizo ya jumuiya kwa sasa kama ilivyo
vigumu kusuluhisha matatizo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Ukitazama
sasa tunapambana kuendeleza Muungano na Zanzibar, hili la nchi zote nne
litakuwaje? Mali zinatoka nchi nyingine, vivyo hivyo kwa upande wa
bidhaa, kwa maana hiyo hatuwezi kufika kwenye shirikisho kabla
hatujamaliza vikwazo hivi vingine,” alisema Sitta.
Tanzania yailima barua EAC
Waziri Sitta pia alieleza kuwa
Tanzania imeiandikia barua sekretarieti ya baraza la mawaziri wa nchi
wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki, ikilalamikia baadhi ya mambo
yanayoendeshwa kwa usiri na baadhi ya nchi katika jumuiya hiyo.
Alisema
barua alikabidhiwa katika kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika
Agosti 28 mwaka huu, mkoani Arusha, ikitaka wahusika kuweka wazi mambo
yanayoendelea ndani ya jumuiya kwa kuzishirikisha nchi zote.
Aidha,
Sitta alieleza kuwa wakati barua hiyo ikiwa imekwishawasilishwa kwa
Sekretarieti, viongozi ambao wamekubaliana kuanza mchakato wa kuandika
Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa, wanapaswa kutambua kuwa
Katiba itakayopatikana itakuwa batili kwa sababu haikuamuliwa na
wananchi wa nchi husika bali watawala.
No comments:
Post a Comment