Serikali kupitia Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imehadharisha mabalozi
wanaowakilisha nchi zao nchini, kuepuka kujihusisha na mambo ya ndani.
Hadhari
hiyo imetolewa jana katika taarifa ya wizara hiyo kwa vyombo vya habari,
baada ya Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China, Lu Younqing, kuonekana
katika mkutano wa hadhara wa CCM, akiwa amevalia kofia yenye nembo ya
chama hicho.
“Wizara inaelekeza kwamba kitendo cha Balozi yeyote
kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, na kuvaa sare zenye
nembo ya vyama vya siasa, sio sahihi na kinakiuka Mkataba wa Vienna wa
mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa
kidiplomasia.
“Mkataba
huo wa Vienna unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na masuala
ya ndani ya nchi, ikiwemo siasa wanapofanya kazi zao katika nchi za
uwakilishi,” ilieleza taarifa hiyo iliyotumwa na msemaji wa wizara hiyo,
Mkubwa Ally.
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa hata Sheria ya
Diplomasia ya Tanzania ya Mwaka 1986, ambayo ni zao la Mkataba wa
Vienna, pia hairuhusu Balozi au mfanyakazi wa Ubalozi, kujihusisha na
masuala ya ndani ya nchi.
“Itakumbukwa kwamba, Katika kipindi cha
mwaka 2010 hadi 2012, Wizara ilikumbana na vitendo vinavyofanana na
kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki, kadhalika kwa tukio hili Wizara
itachukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hili
lisitokee tena,”
“Wizara inapenda kutamka kwamba kitendo cha
Balozi yoyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa
sare zenye nembo ya vyama vya siasa siyo sahihi na kinakiuka Kifungu
cha 41(1) cha Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa
kidiplomasia,” alisema Membe katika taarifa taarifa hiyo.
Lu
alikuwa amevaa kofia yenye nembo ya CCM na alikwenda Shinyanga
kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba,
vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina, Tahong na viwanda hivyo vita kuwa
na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika
mwakani.
Balozi huyo amenukuliwa na vyambo vya habari wakati
akihutubia mkutano wa hadhara akiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana, na kujitahidi kuwasalimia wananchi hao kwa lugha ya kabila la
Wasukuma kwa kusema mwadila.
Alisema pamoja na Tanzania kuwa na
mfumo wa vyama vingi, anaamini kuwa CCM bado iko imara na inaweza
kuendelea kuongoza kwa muda mrefu.
“Kwa hili inadhihirisha kuwa
hakuna chama kama CCM kutokana na uimara wake na hili wanalofanya sasa
la kuja kuimarisha chama nasi kule China kupitia chama chetu tawala cha
CPC (Chama Cha Kikomunisti cha China), tunafanya kama hivi pia. Mwadila,
Shinyanga, CCM Oyeeeeee asanteni sana,” alikaririwa akisema.
Taarifa
hiyo ilisema kuwa Balozi huyo alikwenda wilayani humo kuhudhuria
uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba vinavyojengwa na
mwekezaji wa Kichina anayeitwa Tahong, na viwanda hivyo vitakuwa na
uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika
mwakani.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, imeelezea kutambua uhusiano mzuri uliopo kati ya Jamhuri ya
Watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na vilevile inatambua
kazi nzuri ambayo BaloziLu Younqing amekuwa akiifanya tangu alipowasili
nchini Tanzania.
--- via HabariLeo na NIPASHE
No comments:
Post a Comment