LEMAVU AFICHWA NDANI MIAKA 12 BILA KULIONA JUA.
Ni
umbali wa kilomita saba kutoka katikati ya Mji wa Dodoma upande wa
Mashariki barabara iendayo Morogoro, kipo kijiji maarufu cha Nzuguni.
Katika
Mtaa wa maarufu wa Mapinduzi iko familia ambayo wakati mwingine kwa mtu
wa kawaida unaweza usiamini simulizi yake lakini ni ukweli mtupu kwamba
kuna tatizo katika familia hiyo jambo ambalo linahitaji juhudi za
makusudi kuwasaidia.
Waswahili
wanasema ‘kama hujui kifo basi kachungulie kaburi’ hivyo basi, hali ya
maisha ya familia hii kwa ujumla inahitaji kusaidiwa, wanaishi kwenye
katika kibanda kidogo cha tope.
Ni
katika familia ya Lameck Mwitewe Senyagwa na mkewe Anastazia Alfred
yupo Stephen Lameck (21), kijana ambaye hajui mwanga wa jua la kijiji
hicho ukoje, wala haijulikani ni lini kijana huyo ataishi walau kama
binadamu wengine.
Stephen
(Leba) ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanne wote wakiwa
wa kiume, lakini yeye pekee ndiye ambaye hajawahi kuyafaidi maisha
katika kipindi chote cha uhai wake.
Ni mlemavu wa miguu, mgongo na hazungumzi chochote ingawa kwa ishara anaweza kueleza nini anachotaka kutendewa wakati huo.
Kwa
namna ilivyo, angeweza hata kuendesha baiskeli ya miguu mitatu, lakini
nani wa kumpa baiskeli hiyo ili imsaidie kijana huyo kuona mwanga wa
jua, ni tabu na mateso makubwa juu yake.
Nilifika
katika kibanda kidogo ambacho familia hiyo ya watu sita (watoto wanne
na wazazi wawili wanaishi), inatia huruma lakini ndiyo hali halisi
waliyo nayo, na haikuwa mara ya kwanza kuona maisha duni kama hayo
isipokuwa mateso yapo kwa Stephen.
Simulizi ya mama mzazi
Katika
kibanda hiki, nakutana na mama mzazi wa kijana huyu, mara baada ya
kujitambulisha anaonyesha ushirikiano, isipokuwa anapinga mimi kuingia
ndani huku akitaka historia ya kijana wake niipate nikiwa nje. Baada ya
dakika kadhaa tunakubaliana kuingia ndani aliko Leba.
Nilitaka
kujua historia kamili na yeye alianza kwa kusimulia “Leba ni mwanangu
wa kumzaa, ndiye mtoto wangu mkubwa kati ya watoto wanne,” anaanza
kusimulia Anastazia Alfred.
Mama
huyo anasema kuwa tatizo la kutokutembea kwa Leba halikumuanza hivi
karibuni, bali ni tangu alipokuwa tumboni na lilitokana na tatizo
alilokuwa nalo mama yake mzazi kabla ya kuzaliwa kwa mtoto.
Chanzo cha ulemavu
Anasema tatizo la mwanaye lilianza katika ugonjwa ambao yeye mzazi aliupata wakati akiwa na mimba ya miezi sita.
“Niliambiwa
kuwa ninaumwa kifafa cha uzazi, wakati huo nilikuwa siwezi kufanya
jambo lolote na hata macho yangu yalikuwa hayaoni,” anasimulia
Anastazia.
Mama
huyo anasema mara baada ya ugonjwa huo kumzidi, alipelekwa katika
hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambako alijifungua mtoto wakati huo akiwa na
mimba ya miezi saba.
Anasema
baada ya kujifungua, mtoto alikuwa ni dhaifu kiasi kwamba wengi
walikata tamaa kuwa asingeliweza kupona. Hata hivyo kwa mapenzi ya Mungu
akapona.
Atoroka na kumwacha mtoto
Kwa
maneno yake anasema kuwa alitoroka hospitalini na kwenda kwa ndugu zake
katika Mtaa wa Makole ambako aliwaeleza kuwa asingekuwa tayari
kuendelea kuishi na mtoto ambaye watu walishamwambia kuwa ni mkosi
kuishi naye.
Hata
hivyo, alikumbana na changamoto nyingine kutoka kwa watu ambao
walimtaka arudi tena kwa ajili ya kumchukua mtoto na kwamba wasingekuwa
tayari kumpokea mahali popote kama angerudi bila ya Leba.
“Nilikuwa
nimechanganyikiwa na wakati mwingine utoto ulikuwa bado unanisumbua na
kwa kuwa sikuwa na mama wakati huo ambaye angeweza kunifunda zaidi hivyo
nikaona njia njema ya kunisaidia ni kumtelekeza mtoto,” anasimulia.
Hata
hivyo, anampongeza marehemu baba yake kuwa alikuwa ni msaada mkubwa
kufanya mtoto huyo aendelee kuishi kwani aliposikia mambo hayo, alimwita
kijijini kwao Kwamtoro Wilaya ya Chemba (zamani Kondoa) ambapo
alimketisha chini na kumwonya juu ya tendo hilo.
Anasema
baba yake huyo alimtaka kuishi na mtoto bila ya kumtenga, na akampa
mifano hai ya watu wenye ulemavu ambao wanaishi hadi wakati huo.
Mateso ya mtoto
Mbali
na kukubaliana na kuishi na mtoto huyo, hali ya Leba kwa sasa inatisha,
hana msaada wowote. Hawezi kutoka nje, amekuwa akifichwa ndani kwa
zaidi ya miaka 12 sasa.
Chakula ni tabu, mazingira anayoishi hayaendani na hali yake na haijulikani ni lini atapata nafasi ya kuona mwanga.
Ni
zaidi ya miaka 12 sasa kijana huyo anaishi ndani ya nyumba na watu
wengi hawamjui licha ya kuwa mama yake anajulikana kwa jina la Mama
Leba, mwenye jina majirani hawamjui.
Hiyo
itatokana na kushindwa kupata msaada wowote walau wa baiskeli au hata
njia nyingine, zaidi ya kutegemea mama yake mzazi ambaye anasema kuwa
kijana huyo amekuwa mzito hawezi kumbeba.
Hali ya familia
Maisha
ya familia ya Lameck ni magumu, hawana nyumba, wanaishi katika kibanda
kidogo ambacho wamepewa na mlo wao ni shida, humlazimu baba wa familia
kutafuta kwa bidii huku watoto wote watatu wakimtegema kwa masomo mmoja
akiwa kidato cha nne, mwingine amemaliza darasa la saba na wa mwisho
darasa la pili.
Hata hivyo, upendo wa kuwa pamoja bado umeendelea kuwafanya wasitupane wala kuwa na migogoro.
Nini wanahitaji
Anastazia
anasema kama watapata nafasi ya kusaidiwa baiskeli kwa ajili ya Leba
akaweza kutoka nje, naye angepata nafasi ya kupumua na kutafuta biashara
yoyote ya kumsaidia mumewe kwani kwa sasa hawezi kutoka umbali wa mita
100 na kumwacha mtoto.
Anasema
katika umri wa miaka mitatu wa kijana huyo, walikutana na mtaalamu
kutoka Asia ambaye alisaidiana na wataalamu wa hospitali ya mkoa
kumfanyia mazoezi kijana huyo, kiasi cha kumwezesha kwa sasa akipewa
baiskeli anaweza kuendesha japo kwa shida.
Kwa
sasa ni kama wamepoteza matumaini lakini wanaamini kwa misaada kutoka
kwa wasamaria wema labda hali ya maisha yao inaweza kubadilika na kuwa
nzuri zaidi ya ilivyo sasa.
-Mwananchi
No comments:
Post a Comment