RAIS OBAMA AIMWAGIA SIFA TENA TANZANIA...AMWITA RAIS KIKWETE KUWA RAFIKI WA KWELI...!!
Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama
ametoa pongezi na sifa kwa Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi chache
duniani ambazo zimetia saini mkataba wa Ushirikiano wa Serikali
Zinazoendeshwa kwa Uwazi ambao unalenga kujenga na kuendeleza nafasi ya
taasisi zisizokuwa za Kiserikali katika utawala bora, uwazi na
uwajibikaji katika uendeshaji wa Serikali.
Rais Obama ametoa pongezi
hizo kwa Tanzania leo, Jumatatu, Septemba 23, 2013, wakati akizungumza
katika mkutano maalum aliouandaa mwenyewe Rais Obama kuzungumzia nafasi
za Serikali katika kuunga mkono na kuendeleza asasi na taasisi
zisizokuwa za Kiserikali na kuzishirikisha zaidi katika kuboresha
shughuli za utawala bora uliofanyika kwenye Hoteli ya Hilton, mjini New
York, Marekani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi wachache duniani
walioalikwa kushiriki mkutano huo maalum ambao pia ulishirikisha
wawakilishi wa asasi zisizokuwa za Kiserikali 300.
Baadhi ya nchi
nyingine za Afrika zilizoalikwa na kushiriki katika mkutano huo ni
pamoja na Liberia, Ghana, Benin, Libya, Tunisia, Senegal, Afrika Kusini
na Botswana.
Shabaha kuu ya mkutano huo wa saa moja ilikuwa ni
kutafuta namna ya kuongeza kiwango cha kuungwa mkono kwa taasisi na
asasi hizo na jinsi gani ya kuzilinda ili kuziwezesha kufanya kazi kwa
ufanisi zaidi.
Aidha, mkutano huo ulilenga kuzitaka Serikali ambazo
zinaweka vikwazo kwenye utendaji wa asasi hizo kuondoa vikwazo hivyo
haraka ambavyo vinahujumu utendaji kazi na mchango wa asasi hizo katika
uendeshaji wa utawala bora.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa
mkutano huo, Rais Obama amezisifia nchi kama Tanzania ambazo zimetia
saini makubaliano ya Ushirikiano wa Serikali Wazi ambayo yanalenga
kupandisha nafasi ya asasi zisizokuwa za Kiserikali katika Utawala
Bora,Uwazi na Uwajibikaji katika Serikali.
Amesema kuwa binafsi
alikuwa ameamua kukutana na viongozi wa asasi zisizokuwa za kimataifa
wakati wa ziara yake ya karibu katika Afrika ambako miongoni mwa nchi
nyingine alitembelea Tanzania.
Rais Obama alifurahi sana kukutana na
Rais Kikwete. Rais Obama alimkumbatia Rais Kikwete akimwelezea kama
“kaka wa karibu na rafiki mzuri” kauli na kitendo ambacho kiliwashangaza
mamia ya watu waliokuwa kwenye ukumbi.
No comments:
Post a Comment