Obama kuendeleza shinikizo kwa Syria

Wafuasi wa serikali ya Bashar Al Asad

Rais wa Marekani Barack Obama, amesema kuwa atafanya juhudi zaidi za kidiplomasia kuangamiza zana za kemikali za Syria , lakini pia ameambia jeshi lake kuwa tayari kuchukua hatua ikiwa juhudi zake zitafeli.

Kwenye hotuba yake , Obama alisema kuwa amelitaka baraza la Congress kuakhirisha kura yake kuhusu kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Syria.

Marekani imetishia kufanya mashambulizi ya angani baada ya shambulizi la kemikali kuwaua mamia ya watu mjini Damascus mwezi jana.

Urusi imependekeza kuwa silaha hizi ziwekwe chini ya udhibiti wa jamii ya kimataifa.

Ingawa maafisa wa Syria wamekubali kutii agizo la Marekani, nchi hiyo pamoja na washirika wake wana wasiwasi ikiwa Syria itafanya kama inavyosema.

Athari za vita nchini Syria , watoto hawajasazwa

Mpango wa Urusi ulisababisha siku moja ya mashauriano mazito ya kidiplomasia katika Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne.

Akiongea katika Ikulu ya White House, Obama alisema kuwa serikali yake, ilikataa wito wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria kwa sababu haamini ikiwa kutumia nguvu itasuluhisha mgogoro huo.

Lakini alisema kuwa alibadili msimamo wake baada ya zana za kemikali kutumiwa kwenye mashambulizi katika viunga vya mji wa Damascus tarehe 21 mwezi Agosti.

"usiku huo, dunia nzima iliona kwa kina athari mbaya za zana za kemikali na kwa nini watu wengi duniani wanahisi kuwa zana hizo hazipaswi kabisa kutumiwa, ni uhalifu dhidi ya binadamu na ukiukwaji wa sheria za vita,'' alisema Obama.

Serikali ya Syria imekanusha kuwa ilitumia silaha za kemikali kushambulia watu na badala yake imelaumu waasi ikisema walizitumia katika juhudi zao za kutaka kumng'oa mamlakani Rais Bashar al-Assad


No comments: