Kumekuwa na mjadala mkali kuhusu iwapo Naibu Spika, Job Ndugai
alikiuka Kanuni za Bunge katika kushughulikia vurugu zilizotokea Bungeni
Alhamisi iliyopita kwa kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Ndugai ambaye alikuwa kiongozi wa shughuli za
Bunge siku hiyo, aliwaamuru askari kumtoa nje Mbowe baada ya kukaidi
amri yake ya kutaka kuketi chini aliposimama kutaka kupewa nafasi ya
kuzungumza, hali iliyozua tafrani bungeni.
Pamoja na mambo mengine Ndugai amekuwa akituhumiwa
kwamba anaminya uhuru wa wabunge wa upinzani kutokana na mapenzi
aliyonayo kwa chama chake, CCM.
Kwa upande mwingine, kumekuwa na lawama kwamba
Mbowe alikosea kukaidi amri ya Naibu Spika kwa kuwa kanuni zinamtaka
mbunge yeyote (hata akiwa waziri), kuketi pale kiongozi wa Bunge (Spika,
Naibu au Mwenyekiti) anaposimama, hivyo kusababisha mtafaruku.
Mwenyekiti wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar,
Profesa Chris Peter Maina alisema tatizo lililojitokeza bungeni
linaweza kumalizwa na kuwapo kwa sheria inayokataza Spika wa Bunge kuwa
mwanachama wa chama chochote cha siasa.
“Unajua kwa Katiba ya sasa Spika wa Bunge anaweza
kuwa mwadilifu lakini akapata shinikizo kutoka upande wa chama chake,
Ibara ya 128 ya Rasimu ya Katiba Mpya inaeleza kiundani kuhusu spika
kutokutoka miongoni mwa wabunge jambo ambalo ni zuri,” alisema Profesa
Maina na kuongeza:
“Mwenendo wa Bunge siyo mzuri. Wabunge
hawaheshimiani hata kidogo, nadhani wanahitaji kukubaliana kwa hoja, wao
ndiyo wanatunga sheria, hivyo wanatakiwa kulumbana kwa kufuata
utaratibu uliowekwa.”
Spika wa zamani, Pius Msekwa alisema wakati
akiongoza Bunge hakuwahi kuona vurugu, fujo na malumbano ya wabunge kama
ilivyotokea Alhamisi iliyopita.
“Wakati nikiwa Spika sikumbuki kama kuna siku
ziliwahi kutokea vurugu za aina hii, kilichotokea ni sawa na uhalifu kwa
sababu taratibu hazikufuatwa,” alisema Msekwa.
Matakwa ya Kanuni
Ibara ya 76 (1) na (2) ya Kanuni za Bunge Toleo la
Aprili 2013, zinaeleza jinsi ya kudhibiti fujo bungeni, lakini Ndugai
anakosolewa kwamba hakuzingatia taratibu hizo kushughulikia vurugu za
Alhamisi.
Kanuni ya 76 (1) inasema: “Kwa madhumuni ya
kudhibiti fujo endapo itatokea ndani ya Ukumbi wa Bunge na Spika ataona
kuwa kuna haja ya kutumia nguvu, basi anaweza kuahirisha shughuli za
Bunge bila ya hoja yoyote kutolewa au kusitisha kikao kwa muda
atakaoutaja ili fujo hiyo iweze kudhibitiwa na Mpambe wa Bunge”.
Kadhalika, fasili ya pili ya Kanuni hiyo inasema: “Baada ya
utulivu kurudia, Spika atalipeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge suala ambalo lilisababisha kutokea kwa fujo ikiwa ni
pamoja na jina la mbunge au majina ya wabunge waliohusika na fujo hiyo
ili kamati hiyo iweze kulishauri Bunge kuhusu adhabu inayostahili
kutolewa”.
Wakati vurugu zilipozuka bungeni, Ndugai aliwaita
askari badala ya mpambe, kumtoa nje Mbowe na hakuwa amesitisha wala
kuahirisha shughuli za Bunge kama kanuni zinavyotaka.
Pia Naibu Spika alitangaza kumsamehe Mbowe na
Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwa maana ya
kuwaruhusu kuendelea na vikao vya Bunge siku hiyo jioni, badala ya suala
hilo kupelekwa kwenye kamati husika kama kanuni ya 76 (2)
inavyoelekeza.
Utetezi wa Ndugai
Ndugai alisema hakuzingatia kanuni hizo kwani
mazingira ya vurugu hizo hayaendani na kanuni husika, hivyo alitumia
nafasi yake ambayo pia inatambuliwa na kanuni za Bunge.
“Vurugu zilikuwa zimepangwa na zilifanywa kwa
makusudi ili kuhakikisha kwamba shughuli za Bunge zinakwama maana hiyo
kanuni wanafahamu kwamba ipo, sasa hatuwezi kuwa na Bunge ambalo mtu
akiamua tu anafanya fujo ili liahirishwe,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Mimi kama kiongozi wa shughuli za siku hiyo, kazi
yangu ni kuhakikisha kwamba shughuli zilizopangwa zinafanyika, kwa hiyo
nisingeweza kuruhusu watu wachache watukwamishe kutokana na masilahi
yao.”
Alipoulizwa kwamba alifahamu vipi kuwapo kwa njama
hizo, alisema kauli na matendo ya wabunge wa upinzani vilionekana tangu
mwanzo wa mjadala kutaka kukwamisha shughuli za Bunge siku hiyo.
Kuhusu kuwatangazia wabunge hao msamaha badala ya
kupeleka suala hilo kwenye kamati husika, Ndugai alisema: “Hakukuwa na
adhabu kubwa ya kuwapa zaidi ya kuwatangazia msamaha.”
“Niliwasamehe kwa mujibu wa kanuni maana
zinaruhusu kuzingatia uamuzi ambao uliwahi kutolewa na maspika
waliopita, kwa hiyo kama unakumbuka kesi ya Mengi (Regnald) na Malima
(Adam), Spika Samuel Sitta baada ya kumwita Malima akakataa kwenda
alisema anamsamehe,” alisema na kuongeza:
“Yeye (Sitta) alitumia neno kwamba nimeamua
kumpuuza lakini mimi sikusema hivyo, nilisema kwamba namsamehe kwa
sababu tu namheshimu na ni kiongozi mkubwa tu katika jamii”.
Lissu amtetea Mbowe
Mbowe hakupatikana juzi na jana kuzungumzia suala hilo, lakini
Mnadhimu Mkuu wa Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema kiongozi wake
huyo hakufanya makosa kwani alisimama wakati Mbunge wa Vunjo (TLP),
Augustine Mrema alipokuwa akizungumza na kwamba hilo siyo kosa kikanuni.
Alisema Ndugai alipaswa kumheshimu Mbowe kwa
kuzingatia wadhifa wake bungeni na kwamba kitendo cha kumwambia “kaa
chini” hakikubaliki.
“Hatuwezi kuruhusu na hatutaruhusu Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kudhalilishwa, ikiwa tutaruhusu hilo
litokee, basi miongoni mwetu sisi wapinzani hakuna atakayepona,” alisema
Lissu na kuongeza:
“Naibu Spika amelidhalilisha Bunge kwa sababu kwa kumdharau Mbowe ni kwamba amemdharau mmoja wa viongozi wakuu wa Bunge”.
-Mwananchi