Miaka 50 baada ya kufariki ; Watafiti wagundua kazi zaidi za Shaban Robert
Miaka 50 baada ya kufariki ; Watafiti wagundua kazi zaidi za Shaban Robert
Ukitoa
simulizi isiyovutia ya kusahauliwa kwa Shaban Robert, baada ya utafiti
wa miaka mingi kuna habari mpya za kugunduliwa kwa kazi nyingine za
gwiji huyo. Kazi hizi hazikuwahi kufahamika awali.
Hakuna apingaye kuwa Shaban Robert alikuwa manju wa fasihi ya Kiswahili, ambaye hata baada ya miaka 50 tangu kifo chake mwaka 1962, hakuna aliyejitokeza kumpiku kwa kiwango alichofikia katika fani ya fasihi.
Mpaka sasa kazi zake nyingi bado zinaishi, huku zikiwa zimetafsiriwa katika lugha mbalimbali na kusambazwa kote duniani.
Bila shaka, mtu huyu anabaki kuwa miongoni mwa watu muhimu waliowahi
kutokea nchini. Lakini inashangaza kuwa familia yake na hata historia
yake vimetelekezwa!
Hata mahala lilipo kaburi lake katika
kijiji cha Machui, Kusini mwa Jiji la Tanga, pameshindwa kuendelezwa
japo kwa kuwa na makumbusho madogo ya mwanafasihi huyo aliyetamba ndani
na nje ya mipaka ya Tanzania.
Kimsingi, eneo hili mbali ya kuwa
sehemu muhimu katika historia ya nchi, pia lingeweza kutumika kama
darasa la kuwakusanya watu, hasa watafiti na wanahistoria kutoka pembe
zote za dunia. Ukitoa simulizi isiyovutia ya kusahauliwa kwa Shaban
Robert, baada ya utafiti wa miaka mingi kuna habari mpya za kugunduliwa
kwa kazi nyingine za gwiji huyo.
Kwa mujibu wa mwanafasihi
bobezi nchini, Profesa Mugyabuso Mulokozi, aliyeshiriki katika utafiti
huo, kazi hizi hazikuwahi kufahamika awali.
Anasema katika
utafiti wao mpya wamegundua mafungu ya barua ambayo Shaabani Robert
aliyaweka katika makundi ya nyaraka za kifamilia, kazi na ajira, pamoja
na kiofisi.
‘’Baadhi ya barua zinahusu uhusiano kati ya mtu na
kaka yake. Shaaban Robert alijipa jukumu la kulea, anazungumzia umuhimu
wa mtu kutenda mema na umuhimu wa elimu katika dunia hii’’anabainisha.
Pia anasema katika utafiti huo wamebaini makala za mashairi
alizopeleka kwenye mashindano, na kuwa mashairi hayo bado ni muswada
yakisubiri kuchapishwa.
Misukosuko ya kisiasa
Miongoni
mwa mambo yanayoibua maswali kwa wanafasihi wa sasa ni namna Shaaban
Robert alivyoweza kuepuka misukosuko ya kisiasa, hasa enzi za ukoloni
kwani baadhi ya kazi zake zipo zilizokuwa zikipinga unyanyasaji wa
Waafrika.
Jambo hili pia limebainika katika utafiti huo mpya.
Inadaiwa kuwa katika vita Kuu ya Pili ya Dunia(1939-1945), aliandika
utenzi wa vita hiyo akiisifia Uingereza kuwa ilikuwa na haki dhidi ya
dola ya Wajerumani.
Utenzi huo haukuifurahisha Ujerumani na
gwiji huyo wa fasihi ya lugha ya Kiswahili aliwekwa katika orodha ya
watu watakaonyongwa endapo Wajerumani wangeshinda vita.
Aidha,
kwa mujibu wa Profesa Mulokozi miongoni mwa kazi zilizogunduliwa, ni
sehemu ya utenzi alioandika akilalamikia kuhamishwa vituo vya kazi mara
kwa mara.
Sehemu ya utenzi huo inanukuliwa ikisema:
’Nimezaliwa Tanga 1909, tangu utoto sina kituo hasa, naona sina siasa ila kuandama njia’’
Mashairi mengine yanatajwa kuwa yanaelezea mila za watu wa Tanga.
Katika kazi mpya zilizogunduliwa pia anazungumzia jinsi watu
walivyoweza kupata tiba. Kwa mfano, anasema mtu alipougua alikwenda
kwenye tambiko, msikitini kuombewa au hospitali.
Akimzungumzia
Shaaban Robert, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Felix Sosoo anasema kuwa alikuwa ni mtunzi
aliyeheshimika na ametoa mchango mkubwa kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Mwanafunzi huyo kutoka Ghana anasema amefika nchini kujifunza zaidi
lugha ya Kiswahili na baada ya masomo atarudi Chuo Kikuu cha Ghana kama
mtaalamu wa lugha hiyo.
Anasema anajivunia kusomea katika nchi
anayosema ndiyo chimbuko la lugha ya Kiswahili na kuwa lugha hiyo ni
utambulisho wa utamaduni wa Afrika. Matarajio yake ni kubobea na kuwa
mtalaamu zaidi wa lugha hiyo.
‘’Nimetoka Ghana kujifunza
Kiswahili ambayo ni kama lugha ya Afrika, hapa najifunza Kiswahili
fasaha. Lugha hii itanirahisishia kujifunza lugha nyingine pia’’ anasema
Sosoo
Akitoa maoni yake kuhusu umahiri wa Shaaban Robert,
msanii wa Kimataifa John Mugango, anasema mtunzi huyo ameacha somo kwa
Taifa kuendeleza watu wake kulingana na vipaji walivyonavyo.
Anasema vipaji vingi vinapotea kwa kutoendelezwa na kuwa badala yake
wanapatikana wataalamu wanaofanya kazi kwa shinikizo la kukosa ajira na
siyo kwa sababu ya kupenda kazi husika.
‘’Tusomee vipaji
vyetu, ukiona daktari anakukaripia baada ya kumfikisha mgonjwa
hospitali, ujue huyo ana damu ya ajira katika kazi yake na siyo udaktari
wa kujitambua’’anabainisha Mugango
Naye Mwalimu Domician
Domonick kutoka Shule ya Sekondari Bukoba, anashangaa gwiji huyo
kutopewa shahada ya heshima na taifa, kama sehemu ya kutambua mchango
wake katika kukuza lugha ya Kiswahili.
Anasema Shaabani Robert
ana mchango mkubwa katika kuifanya lugha hiyo iheshimike duniani.
Analalamika kuwa hivi sasa Serikali inapitisha vitabu vya kufundishia
lugha hiyo ambavyo maudhui yake ni dhaifu.
Anasema vitabu
vinavyotumika hivi sasa vingi havina mantiki ya fasihi na kwa vyovyote
haviwezi kulinganishwa na vile vilivyotungwa na Shaaban Robert. Anarejea
baadhi ya vitabu vyake kama vile Mapenzi Bora kinachoonyesha umuhimu
wa elimu.
Kauli ya mtoto wa Shaban Robert
Ikbal Shaaban ambaye ni mtoto wa Shaaban Robert anasema kazi za baba yake hazijasaidia kuboresha maisha ya familia aliyoiacha.
Anaeleza kuwa wapo wajanja wanaofaidika na jasho la baba yao na kuwa
hakuna pato linaloingia katika familia yao kutokana na mauzo ya kazi
hizo.
‘’Bado hatujaona faida ya kazi zake zaidi ya kuitwa
kwenye semina, kuna wajanja wanaonufaika na jasho lake,tuko mbioni
kuanzisha vita mpya dhidi ya kazi za marehemu’’ analalamika.
Ikbal anadai kuwa gwiji huyo wa lugha ya Kiswahili hajapewa heshima ya
kutosha na Taifa, licha ya kuwa kazi zake zinaendelea kutumika
kuendeleza na kuitangaza lugha hiyo.
Kwa hali yoyote ile, huu
ni wakati wa kumuenzi Shaaban Robert kwa kutambua mchango wake kwa
taifa, huku tukiendelea kuwaandaa wanafasihi wengine wa baadaye.