Padri wa Parokia ya Mpendae ya Kanisa Katoliki Zanzibar, Anselmo
Mwang’amba amesema kuwa alimwona mtu aliyemwagia tindikali na
kumsababishia majeraha na kueleza kuwa anashangaa kuona polisi
hawajamkamata hadi sasa.
Akizungumza jana katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, kwenye Wodi namba 16, Kibasila alipolazwa, Padri Mwang’amba
alisema baada ya kumwagiwa tindikali, alimwona mtu huyo akikimbia
kuelekea katika nyumba moja jirani.
“Kwa kuwa mimi nilikuwa na taharuki na maumivu,
sikuweza kuendelea kumfuatilia, ila dereva aliyenikimbilia kunipa msaada
aliniambia kwamba alimwona mhusika akikatiza kwenye uchochoro hadi
alipoingia kujificha kwenye nyumba iliyopo jirani na eneo hilo,”
alisema.
Alisema majeraha aliyoyapata wakati akitokea
katika duka la huduma za mawasiliano ya mtandao la Shine Shine saa 10.15
jioni, ambayo yanamsababishia maumivu makali, hayawezi kumfanya
aikimbie Zanzibar, kwa kuwa hata Yesu Kristo wakati alipokuwa katika
kazi za utumishi duniani alipata mateso makali kuliko yake.
“Nilisomea upadri nikiwa Zanzibar kuanzia mwaka
1976 hadi mwaka 1981 nilipopata upadrisho kamili. Niko huko kwa kazi ya
Mungu wala si mwanadamu, kwa hiyo nikitoka hapa narejea hukohuko,
siogopi, ingawa miaka hiyo nilipokuwa naanza kazi hii hakukuwa na mambo
kama haya,” alisema.
Aliwataka Wakristo wanaoishi Zanzibar kuendelea
kuwa na umoja na upendo pamoja na kuwa makini kwa usalama wao licha ya
matukio magumu yanayowakuta ikiwamo vitisho na kuchomwa moto kwa
makanisa.
Pia aliunga mkono shinikizo la kutimuliwa kazi kwa
Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa kutokana na kushindwa
kuwakamata watu wanaomwagia watu tindikali.
“Huyu bwana alishindwa hata kunijulia hali wakati
nikiwa hospitali huko Zanzibar, tofauti na nilipokuja Bara ambako
Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova walifika kunijulia hali na
kuzungumza nami hospitali.
“Kwa hali hii, naona kwamba tukio langu ni la
kupangwa na litazungumzwa sana lakini baada ya muda halitashughulikiwa.
Atajeruhiwa mwingine tena lakini hatua za dhati za kudhibiti ukatili huu
usiendelee hazijachukuliwa. Mimi ni padri wa tatu kufanyiwa ukatili,”
alisema.
Mapadri wengine ni Ambros Mkenda aliyepigwa risasi na kujeruhiwa wakati Padri Evarist Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi.
Al-Shabaab wanaswa Zenji
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Zanzibar
limewakamata watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa kikundi cha kigaidi cha
Al-Shabaab cha Somalia.
No comments:
Post a Comment