Jeshi la Rwanda lasogezwa mpakani....Majeshi ya SADC yaendelea kujiweka tayari kwa lolote
VIKOSI vya wanajeshi vya Serikali ya Rwanda vyenye silaha za kivita,
sasa vimesogezwa katika eneo la mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Taarifa ya kusogezwa kwa vikosi hivyo
mstari wa mbele katika eneo la mpakani, imetolewa jana na Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Katika taarifa yake hiyo,
SADC imeeleza wasiwasi wake kuhusu hatua ya Rwanda kusogeza mbele vikosi
vyake vya kijeshi vilivyo na zana za kivita kwenye mpaka wake na Kongo.
Mshtuko huo wa SADC umekuja ikiwa ni siku chache tangu MTANZANIA Jumatano iripoti kwa mara ya kwanza juu ya kuwapo kwa
taarifa za Jumuiya hiyo kutuma ujumbe wa onyo kwa Rais Paul Kagame wa
Rwanda kuachana na fikra zozote mbaya dhidi ya Tanzania.
Onyo
hilo, lilitolewa baada ya kupatikana kwa taarifa kuwa Serikali ya Kigali
ilikuwa imepeleka vikosi vyake katika mpaka wake na Kongo, kwa ajili ya
kupambana na waasi.
Ni hatua hiyo ya Serikali ya Kigali ndiyo
iliyoilazimu SADC kutuma ujumbe mkali wa kumuonya Kagame kupitia kwa
mmoja wa mawaziri wa nchi yake, aliyekuwa ameambatana naye kwenye
mkutano wa viongozi wa nchi za Maziwa Makuu uliofanyika hivi karibuni
nchini Uganda, ambao pia ulihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete.
Ikiwa
ni takribani wiki moja baada ya kupatikana kwa taarifa za kutolewa kwa
onyo hilo, jana mtandao wa Fox news ulikariri taarifa mpya ya SADC
kupitia moja ya chombo chake, ikieleza kuzuka kwa hali ya wasiwasi baada
ya kubainika kuwa Rwanda imeviamuru vikosi vyake vya jeshi kusogea eneo
la mpaka wake na Kongo.
Ikitumia maneno ya kidiplomasia lakini
yenye taswira ya kuonya, SADC kupitia taarifa yake hiyo iliyotolewa
katika mkutano wake uliofanyika Namibia na kuhudhuriwa pia na Rais wa
Kongo, Joseph Kabila, ilisema kuwa haifikirii kama Rwanda itajaribu
kuivamia Kongo.
Taarifa hiyo inaitaka Rwanda kushiriki kuleta amani, usalama na utulivu ndani ya Kongo.
Katikati
ya wiki hii, gazeti la MTANZANIA Jumatano likikariri chanzo kimoja
cha habari kilichokuwa kwenye mkutano wa viongozi wa nchi za Maziwa
Makuu uliofanyika Uganda, kuwa ujumbe wa SADC kwa Rwanda alipatiwa mmoja
wa Mawaziri aliyekuwa ameambatana na Rais Kagame muda mfupi baada ya
kukutana na Rais Kikwete.
“Uamuzi wa Tanzania na Afrika Kusini
kupeleka majeshi DRC, ni msimamo wa pamoja wa SADC. Vitisho vyovyote
dhidi ya Tanzania au uvamizi wa kijeshi utachukuliwa ni uvamizi dhidi ya
SADC, hivyo tutakuwa tayari kuingia vitani kupigana upande wa
Tanzania.”
Hatua hiyo ya SADC kuikamia Rwanda, ilithibitishwa na
taarifa ambazo gazeti hili liliziona kwenye mtandao wa Intaneti kupitia
gazeti la The Namibian la nchini Namibia, ambalo liliandika kuwa, Jeshi
la nchi hiyo (NDF), ambalo pamoja na majeshi ya nchi nyingine wanachama
linaunda kikosi maalumu cha Jeshi la SADC, lilikuwa limeanza kushiriki
mazoezi ya Jangwani karibu na Walvis Bay, yatakayodumu hadi Oktoba 15
mwaka huu.
Ilielezwa kuwa wakati mazoezi hayo yakiendelea, Mkuu
wa majeshi ya Namibia (NDF), Luteni Jenerali, Epafras Ndaitwah,
aliwakumbusha wapiganaji hao kuwa kwa sasa wanachama wenzao, wakiwemo
wanajeshi wa Tanzania, wanapambana na maadui wa amani nchini Kongo na
kwamba nao ni lazima wajiandae kwa hali yoyote ambayo haitabiriki.
Vikosi
vya Kongo, vinavyoungwa mkono na vile vya Umoja wa Mataifa vilianzisha
mapambano mapya dhidi ya waasi wa M23 mwishoni mwa mwezi uliopita huko
Kaskazini Mashariki mwa Kongo.
Baada ya kupigana kwa mafanikio
makubwa, SADC ilivipongeza vikosi vya Serikali ya Kongo na Brigedia
inayoongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ya FIB kwa
kuendelea kutumia shinikizo la kijeshi dhidi ya waasi wa M23 na vikosi
vingine vilivyoko Mashariki mwa Kongo.
Tanzania, Malawi na Afrika
Kusini, kwa pamoja zimetoa majeshi yao yanayounda brigedia ya wanajeshi
wapatao 3,000 waliopewa mamlaka ya kupambana na vikosi vya waasi kwa
kutumia nguvu.
Nchi zote hizo tatu zilikuwa zikiwasilishwa katika mkutano huo uliofanyika nchini Namibia.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukiishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo nchi hiyo imekuwa ikiyapinga.
Hata
hivyo, waasi hao katika kujibu mashambulizi wamekuwa wakilishutumu
Jeshi la Kongo kwa kuunganisha nguvu na kikundi cha waasi cha Kihutu cha
FDLR, kinachopambana kutoka Mashariki mwa Kongo ambapo wanajeshi wake
wengi wanaounda kikosi hicho, wanadaiwa kukimbia mauaji ya halaiki ya
Rwanda yaliyotokea mwaka 1994.
Mazungumzo kati ya waasi na
Serikali ya Kongo yalianza tena tangu Jumanne, baada ya kukwama mwezi
Mei, kabla ya kuanza tena sasa baada ya kuibuka mapambano.
Wakati
huo huo, juzi bomu dogo lililorushwa mjini Kigali liliua mtu mmoja na
kujeruhi wengine 14 zikiwa zimesalia siku mbili tu kabla ya kufanyika
kwa uchaguzi wa wabunge.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini
Rwanda, Damas Gatare alisema bomu hilo lilirushwa saa 12:30 jioni,
katika eneo la sokoni lenye watu wengi.
Gatare alisema kuwa watu watatu wamekamatwa kutokana na tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea.
Hakuna
yeyote anayeshutumiwa katika shambulio hili la sasa, lakini katika
matukio mengine mawili kama hayo yaliyotokea mwezi Machi na Julai mwaka
huu Serikali imekuwa ikilishutumu kundi la waasi wa FDLR kuhusika.
Rwanda
inatarajia kufanya uchaguzi wa wabunge kesho, uchaguzi ambao
unatarajiwa kutawaliwa na chama tawala cha Rais Kagame cha Rwandan
Patriotic Front (RPF).
0