ICC yataka Marekani imkamate Rais Bashir

 

Bashir ametishia kumfukuza balozi wa Marekani nchini Sudan

Siku mbili baada ya Rais wa Sudan kuiomba Marekani kumpa Visa ya kusafiri nchini humo kuhudhuria mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, wito umetolewa kwa taifa hilo kumkamata Bashir na kumkamabidhi kwa mahakama ya ICC.

Mkutano huo utafanyika wiki ijayo.

Ombi hilo limetolewa na ICC kwa Marekani na kuitaka impe Visa Bashir na kisha kumkamata na kumkabidhi kwa mahakama hiyo pindi tu atakapotua nchini humo.

Bashir anatakikana na mahakama ya ICC kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu na pia kuamuru mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur.

Marekani ilisema kuwa ilipokea ombi la Bashir kutaka Visa na kulitaja ombi hilo kama la kuudhi na kejeli kubwa kwa taifa hilo. Ilimtaka Bashir kwanza kujikabidhi kwa mahakamya ICC kabla ya kutaka kuingia Marekani.

Hata hivyo Marekani sio mwanachama wa mahakama ya ICC na kwa hivyo , kisheria sio lazima itimize matakwa ya mahakama hiyo juu ya Bashir.

Marekani imekuwa katika msitari wa mbele kutaka Bashir akamatwe kwa madai ya uhalifu dhidi yake ili akabiliwa na sheria za kimataifa

Shirika la habari la Reuters lilisema kua mahakama imeshauri Marekani kumkamata Bashir na kumkabidhi kwa ICC ikiwa ataingia nchini humo.

Vibali viwili vya kumkamata Bashir vilitolewa mwaka 2009 na 2010 kwa madai ya uhalifu dhidi ya binadamu.

Hata hivyo Sudan imepuuza hatua ya ICC kumtaka Bashir kwa makosa ya Darfur wakisema kuwa madai hayo yameongezwa chumvi, na nchi hiyo imekataa kuitambua mahakama hiyo ikisema kuwa ni sehemu ya njama ya nchi za magharibi dhidi ya Afrika.

No comments: