DAKTARI
anayedaiwa kuwa bandia amekamatwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,
Dar es Salaam, akiwa na vitambulisho bandia vya mwanafunzi wa Chuo Kikuu
cha Muhimbili cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) akisomea Shahada
ya Pili.
‘Daktari’
huyo ambaye amekuwa akitafutwa na uongozi wa chuo kwa zaidi ya mwaka
alikamatwa jana asubuhi akiwa hospitalini hapo karibu na jengo kilimo
kitengo cha meno.
Katika
kitambulisho chake cha kupigia kura anatambulishwa kwa jina la Dismas
John Macha aliyezaliwa mwaka 1979 Kilimanjaro na anaishi maeneo ya
Upanga Magharibi, Dar es Salaam.
Gazeti
hili, lilimshuhudia mtuhumiwa huyo akiwa katika kituo cha usalama cha
Muhas na kupekuliwa na askari Polisi wa Muhimbili, Anthony Mwamatepela
na kukutwa akiwa na vifaa vya udaktari .
Baadhi
ya vifaa alivyokutwa navyo ni pamoja na koti jeupe la udaktari na
stetoskopu ambacho ni kifaa cha kusikilizia mapafu yanavyofanya kazi na
mapigo ya moyo.
Pia
alikuwa na begi jeusi lenye aina mbalimbali za dawa, vitambulisho na
karatasi nyingi, lakini alipoulizwa alidai kuwa hizo ni dawa zake.
Macha
alikutwa pia na vitambulisho vitatu tofauti, kimoja kikimtambulisha
kuwa mwanafunzi wa Muhas wa Shahada ya Pili ya Udaktari (Masters of
Medicine ) yenye jina la Macha Dismas kikionesha kusajiliwa kwa namba
60520/2011 na kumaliza muda wake Septemba 30 mwakani. Kitambulisho
kingine kilimtambulisha kwa jina la Macha Rogers anayesoma Shahada hiyo
hiyo ikionesha kuwa anamaliza masomo yake mwakani.
Alikutwa
pia na kitambulisho kinachomwonesha kuwa mwanafunzi wa Shahada ya
Kwanza na kadi ya anuani yenye jina la Amos Nnko ambaye ni Ofisa
Rasilimaliwatu wa Chuo hicho.
Akizungumzia
alivyomkamata askari wa chuo hicho, Fulgence Semfukwe alisema
walimkamata baada ya kupata taarifa za yeye kuwa maeneo hayo na kupanga
mbinu za kumkamata.
Alisema
saa 4.45 asubuhi jana alimkuta kwenye jengo la meno na kumwomba kwa
nafasi yake ya udaktari amsaidie tatizo lake na hivyo waongee pembeni,
naye bila wasiwasi akakubali. Alimwuliza anatibu magonjwa gani naye
kumjibu anatibu maradhi ya aina nyingi na kumwomba kitambulisho na yeye
kumpa cha kwake.
Baada
ya hapo alishituka na kudai kuwa ni daktari wa Mwananyamala na amekuja
hapo kwa ajili ya kuona wagonjwa wake wa dharura ndipo alipokamatwa na
kupelekwa kituo cha Polisi.
Alisema
amekuwa akiwachenga kwa muda mrefu kutokana na kuwa kila walipopewa
taarifa yuko wodi au sehemu Fulani hawakumkuta kwani walipishana naye
baada ya kuvua koti na kuweka kwenye begi lake jeusi.
Akizungumza
na gazeti hili, Macha limweleza mwandishi wa habari hizi kuwa yeye ni
mwanafunzi ambaye anaelewa masuala yote ya matibabu, lakini alifeli
chuoni hapo mwaka jana.
Alidai
kuwa dawa alizokutwa nazo ni zake kwani ana matatizo katika njia ya
mkojo na kifua huku akiamua kufanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha.
“Uwezo wa kutibu ninao na nimesoma katika chuo hiki, lakini mwaka jana nilifeli ndiyo maana nikaamua kuwa hivi,” alisema.
Ofisa
Uhusiano wa Muhas, Hellen Mtui alisema kutokana na kukamatwa na nyaraka
akijitambulisha kuwa mwanafunzi wa ‘Masters of Medicine’, ambaye
anaweza kutibu watu hawana uhakika na idadi ya watu ambao ameshatapeli
hospitalini hapo.
Kuhusu
kusoma Muhimbili, Mtui alikana akisema baada ya kupekua nyaraka za chuo
hawakubaini jina la mwanafunzi wa aina hiyo na katika vyeti vyake
bandia vinaonesha kusainiwa na Mkuu wa Chuo aliyekuwapo kabla chuo
hakijapanda hadhi na kuwa chuo kikuu.
Mtui
alisema baada ya kumkamata na kumpiga picha akiwa na mavazi ya
udaktari, kumpekua na kumhoji walimpeleka katika kituo cha Polisi cha
Selander Bridge kwa mahojiano na uchunguzi zaidi.
-Habari leo
No comments:
Post a Comment