MTOTO ACHOMWA MOTO NA MAMA YAKE KWA TUHUMA ZA KUIBA MAYAI YA KUKU HUKO JIJINI MBEYA....!!


WIMBI la ukatili dhidi ya watoto linazidi kushika kasi jijini hapa baada ya mtoto, Emilly George (7) Mkazi wa kijiji cha Ruanda wilaya ya Mbeya kuunguzwa vibaya mikono na mama yake mzazi, Elisia Mwasile (41) kwa maji ya moto kisha kufungiwa ndani kwa siku saba.

Akizungumza huku akiwa anatetemeka kwa hofu, mama wa mtoto huyo, Elisia alisema kuwa chanzo cha kumchoma mtoto wake ni kutokana na kuchoshwa na malalamiko ya majirani zake waliokuwa wakimtuhumu mtoto huyo kujihusisha na vitendo vya wizi vya kuiba fedha na mayai ya kuku.

 

 Mama mzazi wa mtoto aliyechomwa moto  ELESIA MWASILE[41]  akipelekwa kituoni na wanausalama

  Tukio la mwisho lililosababisha mtoto huyo kuchomwa na maji ya moto ni la hivi karibuni ambapo majirani walimwambia mama huyo kwamba mtoto wake ameiba mayai kutoka kwa majirani zake.

Baada ya kuunguzwa kikatili, mtoto huyo alifungiwa ndani kwa siku saba bila matibabu yoyote hali iliyowafanya majirani kuanza kumtafuta wasijue alipo.

Baada ya kutomuona mitaani, majirani hao walitoa taarifa ofisi ya kijiji ili kubaini alipo mtoto huyo.

Uongozi wa kijiji baada ya kupata taarifa hizo ulifanya upekuzi na kumkuta mtoto huyo akiwa amefungiwa ndani huku akiwa na majeraha makubwa katika mikono yake ndipo taarifa ilitolewa Kituo cha Polisi Mbalizi na mama huyo kukamatwa.

Baada ya kukamatwa mama huyo alikabidhiwa kwa Dawati la Polisi Jinsia na Watoto chini ya Kiongozi wa Wilaya, Pudensiana Baitu na mwenyekiti wake, Mary Gumbo ambaye muda mwingi alikuwa akiangua kilio kutokana na kitendo alichofanyiwa mtoto huyo.

 

Hadi tunakwenda mitamboni mama mzazi wa mtoto huyo alikuwa akihojiwa na Polisi Kituo Kikuu cha jijini Mbeya  na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Mtoto Emilly amelazwa katika Hospitali ya Rufaa wodi namba tano akiendelea kupatiwa matibabu.

Vitendo vya unyanyasaji vimeendelea kukemewa  jijini Mbeya na asasi mbalimbali kutokana na watoto kubakwa, kulawitiwa, kufanyishwa  kazi za ndani na baadhi yao kupata ulemavu wa kudumu ikiwemo kupoteza viungo.

No comments: