Moja ya gari alilokutwa nalo mtuhumiwa.
Jengo ambalo linadaiwa ndiyo kiwanda
hatari cha kubadilisha magari ya wizi, kimefumuliwa na mmiliki wake sasa
hivi yupo nyuma ya nondo akingoja kufikishwa mahakamani.
Benovilla Luhanga, 43, ametajwa kuwa
ndiye mmiliki wa kiwanda hicho na siku ananaswa, alikutwa na magari ya
kihafari matano ambayo yote inadaiwa ni ya wizi.
Vilevile, Luhanga alikutwa na Bajaj moja ambayo imedaiwa nayo ni ya wizi na kwamba alikuwa tayari ameshaibadili rangi.
Luhanga alikamatwa akiwa na mkewe ambaye jina lake halikupatikana mara moja.
Kigogo huyo na mkewe, wanaishi ndani ya
nyumba hiyo iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam, kwa nje huonekana kama
gereji lakini ndani ni makazi ya watu na shughuli za ubadilishaji
magari, Bajaj na pikipiki hufanyika humo.
Luhanga na mkewe walikamatwa baada ya
polisi kuvamia kiwanda hicho, saa 5 asubuhi lakini mchakato wa
ukamataji ulikamilika saa 10 alasiri.
Mchakato wa kuwakamata
uliwagharimu polisi jumla ya saa 5 kukamilika kwa sababu ilibidi kufanya
upekuzi wa hali ya juu kwenye kiwanda hicho ili kubeba kila kitu
kilichoonekana ni cha wizi.
Magari yote yaliyokutwa kwenye
kiwanda hicho pamoja na Bajaj moja, ilidaiwa ni mali za wizi huku tayari
yakiwa yameshabadilishwa rangi na kufungwa namba feki za usajili,
isipokuwa gari moja.
Gari aina ya Nissan Navara lenye thamani ya shilingi milioni 45 alilokutwa nalo mtuhumiwa.
ZA MWIZI ZILIVYOTIMIA
Habari
zinaeleza kuwa kuwa kiwanda hicho kiligundulika kutokana na kijana mmoja
ambaye aliwahi kuibiwa gari aina ya Toyota Canter, Goba, Dar, hivi
karibuni.
Imebainika kuwa kijana huyo baada
ya kuporwa gari hilo ambalo yeye alikuwa ameajiriwa kama dereva, maisha
yalimwendea kombo kabla ya kwenda kwa Luhanga kuomba kazi, akidhani ni
gereji.
Chanzo chetu kilitamka kuwa akiwa
ndani ya kiwanda hicho, kijana huyo aliliona hilo Toyota Canter ndani
ya uzio wa kiwanda hicho, hivyo kutoa taarifa Kituo cha Polisi Kawe,
Kinondoni, Dar.
“Baada ya kuripoti, askari
walifuatilia na kukuta kweli kuna gari aliloibiwa kijana huyo na
walipofanya upekuzi wakayakuta magari mengine matano yaliyoripotiwa
kuibwa,” kilisema chanzo hicho.
Habari zinasema, polisi waliweza
kubaini kuwa magari hayo baadhi yake yalibadilishwa rangi na kupakwa
nyeusi huku namba za usajili nazo zikiwa zimebadilishwa.
Nyumba anayoishi kigogo huyo.
KAMATAKAMATA IKAANZA
Polisi baada
ya kugundua wizi huo, kamanda aliyeendesha oparesheni hiyo ambaye jina
lake halikufahamika mara moja, aliamuru Luhanga na mkewe wakamatwe na
magari yaliyokuwa na uwezo wa kutembea yaliendeshwa, mengine yalikokotwa
kwa ‘breakdown’ hadi Kituo cha Polisi Kawe.
Uchunguzi umebaini kuwa watuhumiwa hao tayari wamefunguliwa jalada katika kituo hicho kwa namba KW/RB/8194/2013 WIZI WA MAGARI.
Waandishi wetu walipofika kituoni Kawe Jumapili iliyopita, walikuta ndugu sita wa Luhanga wakihaha kutaka kuwawekea dhamana.
MAGARI YALIYOIBWA
Magari
yaliyoibwa ni aina ya Nissan Navara lenye thamani ya shilingi milioni
45, lililokutwa na kibao cha usajili namba T519 BNP.
Lingine ni Toyota Harrier, ambalo
thamani yake ni shilingi milioni 30. Hili lilikutwa na namba za usajili
T 924 AXB, wakati kuna Toyota Rav4 new model, lenye thamani ya shilingi
milioni 40 ambalo lilikutwa na namba T 581 BBL.
Gari lingine ni Toyota Canter,
vilevile kulikuwa na Rav4 new model nyingine lenye rangi ya kijivu, hili
lilikuwa limeng’olewa namba zake halisi bila kuwekewa nyingine.
Rav4 hilo ambayo halikufungwa
namba, imeelezwa lilikuwa halijabadilishwa rangi, kwani kwa kawaida yale
yanayoporwa na kuingizwa kiwandani humo, hupakwa rangi nyeusi.
OFISINI KWA KAMANDA WA POLISI
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, ACP Camillius Wambura, hakuweza
kupatikana licha ya waandishi kufika ofisini kwake. Hata hivyo, ofisa
mmoja mwandamizi wa jeshi hilo, alithibitisha kutokea kwa tukio.
“Tukio hilo lipo na tunaendelea
na uchunguzi,” alisema ofisa huyo huku akiomba asiandikwe jina lake kwa
kuwa siyo msemaji wa jeshi hilo.
No comments:
Post a Comment