MWANDISHI WA HABARI WA ITV/RADIO ONE ALOPIGWA SHABA NA MZAZI MWENZAKE AANIKA KILA KITU.KUMBE ALIPATA MATESO MAKUBWA SANA KUOKOA MAISHA YAKE.
MWANDISHI
wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro ambaye hivi karibuni
alikumbwa na madhila ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na mzazi
mwenzie, ameanza kufunguka kidogo kidogo na kueleza kwa kina jinsi tukio
zima lilivyotokea.
Akizungumza
kwa sauti ndogo na taratibu na gazeti hili kando ya kitanda alicholazwa
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, mwanahabari huyo alieleza
kushangazwa na ujasiri na nguvu za aina yake ambazo zilimwezesha
kutambaa na kujiburuza hadi eneo la karibu ya barabara ili kuomba msaada
wa kukimbizwa hospitali.
Ufoo
ambaye alionyesha dhahiri kutofurahishwa na baadhi ya taarifa
zinazozingira tukio lake, alisema tayari alikuwa amewahakikishia polisi
waliofika kumjulia hali hospitalini hapo kwamba alikuwa akisubiri afya
yake iimarike kabla hajaeleza kwa kina kila anachokijua kuhusiana na
tukio hilo.
“Alifika
hapa kunijulia hali na kuangalia maendeleo yangu afande Msangi na
nikasema nitakuwa tayari kueleza kila ninachokijua baada ya afya yangu
kuimarika. Nasikitika kuna watu wanasema mambo wakifikia hatua ya kutaka
kuonekana wananifahamu vizuri kuliko hata ninavyojifahamu mwenyewe,”
alisema akionyesha kutofurahishwa na baadhi ya taarifa zinazoripotiwa
kuhusu sakata lake.
Ufoo
ambaye alifikishwa hospitalini hapo Jumapili ya wiki iliyopita kutokana
na kujeruhiwa kwa risasi na mwanaume aliyezaa naye mtoto mmoja alisema
anamshukuru sana Mungu kwa uzima alionao sambamba na kuelezwa kupata
faraja kubwa na kutiwa moyo na mwajiri wake, ndugu, jamaa na
marafiki.
Mwanahabari huyo ambaye bado yuko chini ya uangalizi
wa karibu wa madaktari baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa risasi
mwilini mwake siku chache zilizopita, amelazwa katika chumba cha peke
yake ambacho ingawa kina seti ya televisheni alisema alikuwa haruhusiwi
kuiangalia kwa ushauri na maelekezo ya madaktari.
Huku akionekana
wa chini ya uangalizi mwingine wa karibu na wa kudumu wa muuguzi ambaye
muda wote wa mazungumzo haya alionekana kuwapo katika chumba hicho,
Ufoo alisema alikuwa ana mapenzi makubwa kwa mzazi mwenzake huyo ambaye
alipoteza maisha katika tukio hilo.
“Nilimpenda sana Antheri.
Alikuwa kijana mtaratibu na mpole sana. Najua kile kilichotokea ni
shetani tu na binafsi nilishasamehe alfajiri ile ile baada ya tukio
lile,” alieleza Ufoo ambaye pia alimpoteza mama yake mzazi katika mkasa
huo.
TUKIO ZIMA LILIVYOTOKEA
Ufoo ambaye mara kadhaa
katika mazungumzo na gazeti hili alionekana kukunja uso akiashiria
kupata maumivu, alionyesha eneo la chini ya bega katika mkono wake wa
kulia lililofungwa na bandeji ambalo alisema ndipo alipopigwa risasi ya
kwanza wakati akigeuka na kujaribu kuepuka mauti muda mfupi baada ya
Antheri kumfyatulia risasi zilizomkuta mama yake mzazi.
Akijaribu
kuvuta kumbukumbu ya tukio lilivyoanza, Ufoo alisema mzazi mwenzake
huyo alifika nyumbani kwake akitokea Sudan alikokuwa akifanya kazi usiku
huo huo wa tukio na akamtaka kwenda kwa mama yake (Ufoo) eneo la
Kibamba, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Kabla ya kufika
Kibamba na kwa sababu ambazo Ufoo hakuzieleza, alimkariri mzazi mwenzake
huyo akisema alikuwa amefikia uamuzi wa kujiua yeye na mtoto wao.
“Hata
sijui ni nini kilitokea. Wakati tukitoka nyumbani Antheri alianza kwa
kuniambia kwamba alikuwa amepanga kujiua yeye na mtoto wetu,” alisema
Ufoo kabla ya kukaa kimya kwa sekunde kadhaa na kuendelea na simulizi
yake ya kusikitisha.
Akiwa na sura ya ujasiri, Ufoo anasema
pamoja na kumwambia maneno hayo bado Mushi alimsisitiza kwamba waende
kwa mama yake (Ufoo) baadae warudi kumchukua mtoto wao japo Ufoo
hakusema walitaka kwenda wapi baada ya hapo.
Alisema walipofika
nyumbani kwa mama yake walikwenda moja kwa moja sebuleni na wakiwa
wamekaa kwenye makochi baada ya salamu za hapa na pale ghafla Mushi
akasimama akamwambia mama yake Ufoo kwamba; “Mama nimeishafanya
maamuzi”
Kwa mujibu wa maelezo ya Ufoo, baada ya Mushi kutamka
maneno hayo ghafla akaingiza mkono nyuma ya suruali alikokuwa ameweka
bastola yake na kisha akaichomoa.
Katika maelezo yake Ufoo
alisema baada ya kuichomoa bastola hiyo mama yake naye alisimama na
kwenda kujaribu kumpokonya, kitendo hicho kilimfanya amiminiwe risasi
mfululizo.
Alisema kuona hivyo aliamua kukimbia kuelekea jikoni
ambapo Mushi alimuona na kuanza kumiminia risasi ambayo moja ilimpata
eneo la mkono wa kulia ambayo ilitokezea mbele na kuchana titi la kulia.
Kwa
mujibu wa Ufoo jeraha hilo halikumfanya akate tamaa ya kunusuru maisha
yake kwani alijaribu kukimbia ingawa Antheri alifyatua risasi nyingine
kadhaa ambazo zilimpata juu kidogo ya mgongo na kutokea tumboni ambazo
zilisababisha aanguke chini
Akiendelea kusimulia, anasema ingawa
alikuwa akivuja damu nyingi, na huku akijiburuza ardhini, Ufoo alisema
wakati akitambaa aligeuka nyuma na akamuona Antheri akijielekeza bastola
eneo la kidevu na alipofyatua risasi alianguka chini.
“Nikiwa
chini nilimuona Antheri akijipiga risasi kidevuni na akaanguka chini,
sikujua kilichofuata baada ya hapo kwani niliendelea kujiburuza ili
kuokoa maisha yangu,” alisema Ufoo
ALIVYOJIOKOA
“Nyumbani
kwetu, pale Kibamba si mbali sana na barabarani, wakati nikikaribia
kufika barabarani wakati huo nikitokwa na damu nyingi huku nikihisi
tumbo langu limejaa sana nilikutana na dada mmoja ambaye nilimuomba
khanga ili nijifunge kuzuia damu zisitoke kwa wingi”.
Anasema dada yule alimpa khanga akajifunga na aliposogea barabarani alikutana na gari lililokuwa likiendeshwa na mwanamke mmoja.
“Nilipoona
kuna gari linapita nikainuka kuomba msaada. Liliposimama nilimuona
mwanamke akiendesha nikamweleza kwamba nilikuwa nimepigwa risasi na
nilikuwa nikiomba msaada wake anikimbize hadi katika hospitali ya Tumbi
na kwamba akifika pale tu aniache mlangoni.
“Si rahisi kuamini,
yule mama alikataa kunisaidia akisema alikuwa akiwahi sehemu kumchukua
mzazi. Sina la kusema niliamua kumsamehe tu yule mama ingawa niliumia
sana,” alisema Ufoo.
Alisema muda mfupi tu baadaye alitokea
kijana aliyekuwa na pikipiki, maarufu kwa jina la bodaboda ambaye
alimuomba msaada wa kumkimbiza hospitali ya Tumbi na akakubali.
“Yule
kijana aliniuliza iwapo nilikuwa ninao uwezo wa kujishikilia vizuri na
niliposema nitaweza akanisaidia kupanda katika bodaboda.
“Wakati
huo nilikuwa naona kama tumbo linazidi kujaa. Nikiwa kwenye pikipiki
kuna wakati nilikuwa nikihisi kwamba naweza nikaishiwa nguvu na kuanguka
katika barabara na kisha kupitiwa na gari na kupoteza maisha. Lakini
nilipata ujasiri na kujishikilia,” alieleza kwa sauti ya chini.
Alisema
anakumbuka wakati walipofika eneo la Kibaha ilipo mizani ya kupima
uzito wa magari makubwa walikuta barabara ikiwa imejaa magari na yeye
alimuomba dereva huyo wa bodaboda kupita hata nje ya barabara eneo la
nyasi ili kumwahisha hospitalini jambo ambalo kijana yule alilifanya.
“Nilipofika
eneo la mapokezi pale Tumbi nilimueleza muuguzi niliyemkuta kwamba
nilikuwa nimejeruhiwa kwa risasi na nikamuomba asaidie kuokoa maisha
yangu. Yule nesi alisita akitaka kwanza kupata kibali cha polisi (PF3)
lakini nikaumuomba apigiwe simu, Kaimu Mganga Mkuu wa Tumbi, Dk. Dattan
ambaye tunafahamiana”
“Baada ya muda mfupi Dk. Dattan alifika na
nikamweleza yaliyonipata na mara moja nikaanza kuhudumiwa kwa kuniwekea
dripu, na nikamsikia akiwaeleza wauguzi kwamba isingekuwa busara kwa
hali niliyonayo kama wangeanza kuchukua picha za X-ray kwani hatua hizo
zingeweza kusababisha kupoteza maisha,” alieleza akikumbuka yaliyojiri
hapo Tumbi.
Kwa mujibu wa Ufoo, akiwa bado ana fahamu alimsikia
daktari aliyekuwa akimhudumia akiomba msaada wa gari la kubeba wagonjwa
ili limchukue na kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wito
ambao ulijibiwa kwa maelezo kwamba lilikuwa halina mafuta.
Majibu
hayo kwa mujibu wa Ufoo, yalisababisha daktari huyo aombe kuletewa gari
la wagonjwa la wagonjwa maarufu (VIP) ambalo lililitwa na muda mfupi
baadaye akapakizwa tayari kwa safari ya kukimbizwa Muhimbili.
Alisema
wakati akikimbizwa Muhimbili anakumbuka namna alivyokuwa akipatwa na
maumivu makali wakati wote gari ile ya wagonjwa ilipokuwa ikipanda
matuta ya barabarani na kuna nyakati alikuwa akihisi kupoteza pumzi na
kuishiwa nguvu.
No comments:
Post a Comment